Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 23 Julai, 2017 ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Nguruka uliopo katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma na kufungua miradi miwili ya barabara za Kaliua – Kazilambwa na barabara ya Tabora – Ndono – Urambo.
Mradi wa Maji wa Nguruka ambao utakamilika tarehe 31 Desemba, 2017 utagharimu Shilingi Bilioni 2.87 na ni miongoni mwa miradi 1,810 ya maji inayotekelezwa na Serikali kwa kutumia fedha za mfuko wa maji nchi nzima ambapo mpaka sasa miradi 1,333 kati yake imekamilika na miradi 477 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Barabara ya Kaliua – Kazilambwa ina urefu wa kilometa 56 imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 61.86 na barabara ya Tabora – Ndono – Urambo yenye urefu wa kilometa 94 imejengwa gharama ya Shilingi Bilioni 118.96, fedha za miradi yote miwili zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na wananchi katika sherehe za miradi hiyo pamoja na wananchi waliokuwa wakisimamisha msafara wake katika vijiji vya Uvinza, Mpeta, Usinge, Isawima, Igagala, Ndono, Kalola na Ilolangulu, Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli alimuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kuhakikisha barabara za Urambo – Kaliua yenye urefu wa kilometa 28 inaanza kujengwa ndani ya mwezi mmoja na barabara ya Nyahua – Chaya yenye urefu wa kilometa 85 inaanza kujengwa ndani ya mwezi mmoja na nusu kwa kiwango cha lami.
Mhe. Rais Magufuli pia amewahakikishia wananchi wa Uvinza kuwa Serikali imeshapata fedha za kujenga barabara ya Uvinza – Malagarasi yenye urefu wa kilometa 50 na amemuagiza Waziri Mbarawa kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Kazilambwa – Chagu yenye urefu wa kilometa 41.
Mhe. Rais Magufuli alisema Serikali imeweza kutekeleza miradi hiyo kwa fedha zake inazozipata kutokana na makusanyo ya kodi hivyo amewataka Watanzania kuhakikisha wanalipa kodi ipasavyo na wanadai risiti kila wanaponunua bidhaa na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kukabiliana na mianya yote ya upotevu na matumizi mabaya ya fedha za Serikali.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi hao kuhifadhi mazingira kwa kujiepusha na vitendo vya ukataji miti katika maeneo ya hifadhi na kupunguza idadi kubwa ya mifugo inayozidi uwezo wa maeneo ya malisho waliyonayo na amekataa ombi la wananchi wa Kijiji cha Isawima waliotaka kuongezewa eneo la Kijiji hicho kwa kilometa 20 zaidi kuingia hifadhini.
Kuhusu tatizo la soko la tumbaku linalowakabili wakulima wa zao hilo mkoani Tabora Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wakulima kuwa na subira kwa kuwa Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa imeanza kushughulikia tatizo hilo.
Katika ziara ya hiyo Mhe. Rais Magufuli aliongozana na Mawaziri wawili Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Prof. Joyce Ndalichako, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Daniel Nzanzugwanko na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambao wamempongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali na wamesema wanaunga mkono juhudi hizo.
Leo tarehe 24 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Tabora ambapo ataweka jiwe la msingi la mradi wa maji kutoka ziwa Victoria, atafungua mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora eneo la Kaze-Hill, atafungua barabara za Tabora – Nyahua na Tabora – Nzega na atazungumza na wananchi katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mjini Tabora.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tabora
Chapisha Maoni