Rais wa Jamuhuri wa Muungano Wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amempongeza aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila kutokana na namna alivyojitoa katika kutetea maslahi ya Watanzania kwenye sakata la Escrow(IPTL) na kuonesha uzalendo mkubwa ambao hawezi kusahaulika katika historia ya Tanzania.
Rais Magufuli ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kata ya Nguruka katika hafla ya uzinduzi wa mradi mkubwa wa maji uliopo Tarafa ya Nguruka katika Wilayani Uvinza ambapo alisema kuwa akiondoka hapo bila kumpongeza Kafulila atakuwa amefanya dhambi ya unafiki itakayompeleka motoni.
Akizungumza, Rais alisema anatambua kwamba Kafulila yupo chama kingine, lakini kwenye suala la IPTL, aliweka maslahi ya Taifa mbele na kusimamia ukweli hivyo anampongeza na pongezi hizo ni za dhati kwani zinatoka moyo. Rais alieleza umma uliokuwa umejitokeza mahali hapo kuwa, wizi uliokuwa unafanywa na IPTL ni mkubwa hivyo Kafulila alisimama kutetea umma wa watannzani.
Lakini pia Rais alieleza vikazwo ambavyo Kafuli alikutana navyo wakati akipambana kuhusu wizi huo uliokuwa ukiratibiwa na baadhi ya watumishi wa serikali kwa manufaa yao wenyewe.
“Wakamtisha wengine kumpeleka mahakamani, wakamtukana wee, wengine wakamuita tumbili, sasa tumbili amefanya makubwa kwa ajili ya Watanzania. Wao ndio matumbili, huyu (Kafulila) alifanya kazi ya Mungu ya kuwatumikia Watanzana,” alisema Rais Magufuli huku wakazi wa eneo hilo wakilipuka kwa furaha.
Akiendelea kumwaga sifa hizo za dhati, Rais Magufuli alisema kwenye hili suala la wizi wa IPTL, atampongeza Kafulila kwa maisha yake yote.
Akizungumzia suala la uzalendo, Rais amesema nchi ilikosa uzalendo na kwamba kila aliyekuwa akichaguliwa alikazana kukusanya mali zake yeye mwenyewe bila kujua kuwa atakufa na atazikwa kwenye shimo moja, hivyo akawasihi watanzania wajenge uzalendo.
Alisema maendeleo hayana chama na kwamba, kiongozi mzuri ni yule anayewatumikia watu wake bila kujali chama, kwani mradi huo wa maji anaoufungua utanufaisha watu wote hata wasio na chama. Alieleza kwamba, ushabikia wa vyama ndio unaochelewesha maendeleo ya watanzania.
Rais Magufuli amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku tatu Mkoani Kigoma kwa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa Maji mkubwa katika kata ya Nguruka uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 2 ambao unatarajiwa kukamilika Disemba 30 mwaka huu ambao utafuta kero ya maji kwa wananchi wa kata ya Nguruka.
Chapisha Maoni