ZIARA ya siku tisa ya Rais John Magufuli katika mikoa ya Ukanda wa Kati na Magharibi nchini, imefanikisha kuzinduliwa kwa kilometa 707 za barabara zinazounganisha mikoa zilizojengwa kwa lami kwa gharama ya Sh bilioni 860.
Sherehe za uzinduzi wa miradi hiyo ya barabara zilifanyika katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na kuhitimishwa jana mkoani Singida. Uzinduzi wa barabara hizo unafungua fursa sasa kwa mikoa hiyo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii si kwa Tanzania pekee, bali pia kuiunganisha mikoa hiyo na nchi za jirani.
Akizungumza na wananchi wa Itigi mkoani Singida katika sherehe za uzinduzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya yenye urefu wa kilometa 89.3 jana, Rais John Magufuli alisema serikali yake imedhamiria kuhakikisha mtandao wa barabara kuu nchi nzima unaboreshwa na zote kuwa na kiwango cha lami.
Alitaja barabara hizo na kilometa zake ambazo tangu aanze ziara hiyo alizizindua kuwa ni pamoja na barabara ya Kagoma-Biharamulo- Lusahunga yenye urefu wa kilometa 154 iliyogharimu kiasi cha Sh bilioni 190na barabara ya Kibondo- Nyakanazi kilometa 54 yenye gharama ya Sh bilioni 48.57.
Barabara nyingine alizozindua ni barabara ya Kidawe-Kasulu yenye urefu wa kilometa 63 itakayogharimu kiasi cha Sh bilioni 66.331, Kaliua- Kazilambwa kilometa 56 iliyojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 61.7 na barabara ya Urambo-Ndono-Tabora kilometa 94 iliyogharimu kiasi cha Sh bilioni 118.96.
Aidha, barabara nyingine zilizozinduliwa na Dk Magufuli katika ziara hiyo ni pamoja na Tabora-Nzega yenye urefu wa kilometa 114.9 imejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 160.515, barabara ya Tabora-Nyahua ya kilometa 85 iliyogharimu kiasi cha Sh bilioni 123.773 na Manyoni-Itigi-Chaya ya kilometa 89.3 iliyogharimu kiasi cha Sh bilioni 114.
Alisema barabara zote hizo na nyingine zilizojengwa na zinazoendelea kujengwa utekelezaji wa miradi hiyo ilianzia chini ya uongozi wa marais wa awamu zilizopita na inayoendelea akiwemo Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na mwenyewe Dk Magufuli kwa kutumia fedha za Serikali.
Alisema tofauti na miaka ya nyuma kwa sasa mikoa mingi imeunganishwa kwa barabara za lami na hivyo kuboresha mazingira ya kibiashara na kurahisishia wananchi usafiri. Alisema anashukuru kuwa pamoja na kuwa Rais kwa sasa miradi mingi ya barabara inayotekelezwa kwa sasa ilikuwa chini yake kipindi alipokuwa Waziri wa Ujenzi chini ya serikali ya awamu ya tatu nay a nne hivyo inaifahamu vyema.
Alisema pamoja na ujenzi wa barabara hizo pia mikoa mingi imeunganishwa kwa barabara za lami ambayo hapo awali hali yake ilikuwa mbaya akitolea mfano barabara za Dodoma- Iringa yenye kilometa 261 ilishamikilika, Dodoma-Babati, Singida-Babati-Minjigu na Songida-Mwanza n azote zilijengwa kwa fedha za serikali.
Alimuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa MakameMbarawa ahakikishe ndani ya siku 45 kuanzia jana wakandarasi wanaanza ujenzi wakuilamizia barabara hiyo. Alisema serikali imejipanga kuhakikisha inawaletea maendeleo watanzania bila kujali itikadi zao.
“Hata hizi barabara tunazojenga wale wanaotupinga wanapita humu humu. Dk Magufuli pia aliwataka Watanzania sasa kuanza kujiandaa kuzoea mambo ya kisasa kwani serikali hiyo inatarajia kujenga miundombinu ya kisasa ikiwemo usafiri wa ndege na reli ya mwendokasi inayotumia umeme.
Alisema kuanzia mwakani pia serikali inatarajia kuleta ndege kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 itakayokuwa inatoka Tanzania kwenda moja kwa moja Marekani.
Hata hivyo, Rais huyo alitumia fursa hiyo kumtaka Profesa Mbarawa aingilie kati ujenzi wa mradi wa barabara ya Itigi-Makongorosi yenye kilometa 57 ambayo mkandarasi ametaka alipwe kiasi cha Sh bilioni 104 kiwango ambacho ni cha juu kuliko kawaida.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top