Rais Magufuli, amesema kuwa suala la maendeleo halina itikadi kwani yanayofanywa na Serikali yake hata mtoto wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) atanufaika nayo.
Kutokana hali hiyo alisema bado ataendelea kuwafanyia kazi Watanzania, huku akipambana na watu wanaohujumu rasilimali za Taifa.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Itigi Manyoni mkoani Singida, ambapo alisema hatobagua vyama ila kwa sasa Tanzania inahitaji maendeleo ya kweli na si maneno.
Kiongozi huyo wa nchi alisema anashangazwa na baadhi ya watu kupiga kelele wakiwa jijini Dar es Salaam wakati majimbo yao hayana watu wa kuwasemea kwa kukosa maji, umeme na huduma za afya.
“Ukiona makelele yanapigwa ujue ni rushwa waliyopewa na hao watu..kama ni mmoja, wawili watatu ninawaambia wawekeni kiporo ili muwamwage katika uchaguzi ujao.
“Maendeleo ni ya wote awe mtoto wa nani au mtoto wa nani hata mtoto wa Tundu Lissu. Mna matatizo mengi mahosipitali na mengine lakini hamna wa kuwasemea badala yake wanazungumzia ya Dar es Salaam. Acha mkome si mlichagua wenyewe!
“Kosea njia usikikosee kuoa mke, usije pia kukosea kuchagua na kukosea madhara yake ni makubwa. Mwaka 2020 ikifika msikosee tena,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na hali hiyo alisema kama kuna tochi inawaka basi ina betri“Ukiona mtu anapiga kelele ujue kuna kitu amemeza na sio kingine bali ni rushwa, ukiona tochi inawaka ujue kuna betri,” alisema.
Alisema kuhusu ujenzi wa barabara hiyo itatumia na watu wote wakiwemo wanachama wa Chadema, ACT-Wazalendo jambo ambalo siku zote husimamia dhana maendeleo hayana chama.
Alisema ndani ya Serikali kuliwa na watu watumbuaji kwa kuwa na safari kila kukicha ikiwemo kufanya semina kila mahali ikiwemo nchi za Ulaya huku Watanzania wakiendelea kuumia kwa kukosa maendeleo.
“Nimeamua kuanza na watu wa juu na ninawatumbua kweli kweli kazi ni ngumu unaweza kutumbua ukakutana na usaha ukakurukia kwenye macho.
“Niombeeni nitumbue salama nisije kutumbua watu ambao hawatakiwi kutumbuliwa,” alisema.
Chapisha Maoni