Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Chengula alisema Agosti mwaka jana alijifungua mtoto ambaye aliambiwa katika Zahanati ya Ifisi iliyoko Mbalizi Mbeya Vijijini kuwa mtoto huyo ni wa kiume, lakini siku zinavyozidi kwenda hajui ni wa jinsi gani baada ya maumbile yake ya siri kuwa hayaeleweki ni ya kike au ya kiume. Chengula alisema alipompeleka hospitali huko Mbeya aliambiwa kuwa tatizo hilo ni mpaka ampeleke Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), lakini kutokana na hali yake ya maisha kuwa duni, hakuwa na uwezo wa kufika Dar es Salaam iliko hospitali hiyo.
“Hali hii ilinichanganya sana nikaenda kuomba msaada Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, walinisaidia nikachangiwa pesa kwenye ofisi yao ikapatikana laki mbili na orobaini, nikapewa kwa ajili ya safari pamoja na barua ya rufaa, hata hivyo pesa hizo ziliibiwa zote pamoja na begi langu nikiwa safarini kuja Dar es Salaam,” alieleza msichana huyo. Akielezea maisha yake, alisema mama yake ni mlemavu wa mikono na miguu ambaye hawezi kujishughulisha na kitu chochote na yeye na mama yake wanaishi kwa ndugu yao ambaye anafanya vibarua vya kubeba mizigo ya watu sokoni Mbalizi.
“Maisha yangu ni ya shida sijui nitapataje msaada wa mtoto huyu ambaye nimeambiwa Muhimbili anatakiwa kufanyiwa vipimo na baadaye kufanyiwa upasuaji na mimi sina mtu yeyote wa kunisaidia,” alisema Chengula kwa masikitiko. Aliongeza kuwa pamoja na kwamba hana uwezo wa kumsaidia mtoto wake, lakini anaamini atapata msaada mtoto wake aweze kuwa kama watoto wengine ingawa baba wa mtoto huyo alimkimbia baada ya kuambiwa mtoto ana tatizo.
“Baba wa mtoto alisema hamtaki mtoto na nisimpe jina lake mtoto huyu ni mkosi hataki kujihusisha naye, nahangaika peke yangu nikipata watu wa kunisaidia nitashukuru kwa sababu mimi naamini sio mkosi na atapona,” alieleza msichana huyo. Aidha, alisema katika kipindi chote hicho amemlea mtoto wake kama wa kiume na alimpa jina la kiume ingawa hajui jinsi yake.
“Kipindi chote hicho mimi namlea kama mtoto wa kiume kwa mavazi na jina nimempa la kiume, sasa nikiambiwa ni wa kike sijui nitaenda kuwaambia nini watu kule nyumbani, nadhani nitahama kabisa na sijui nitaenda wapi maana hawatanielewa,” alibainisha. Watoto kuzaliwa na jinsi mbili au isiyoeleweka Daktari Bingwa wa Upasuaji kwa Watoto, Zaituni Dkhary akizungumzia tatizo hilo, alisema mzazi yeyote anaweza kupata mtoto wa namna hii na kwamba tatizo hilo sio mkosi.
Dk Dkhary alisema wazazi mwanzoni huwa wanachanganyikiwa kwa sababu hawajui kama wataweza kuwa kawaida yaani wa jinsi moja walivyo watu wengine au la, lakini tatizo hilo lina ufumbuzi. “Na hakuna kesi yoyote ambayo tumeipata mzazi kurudi kulalamika kwamba kuna hali tofauti imetokea baada ya kuwasaidia, hapa Muhimbili tunawafanyia upasuaji vizuri kabisa kuwarekebishia maumbile na wanakuwa sawa kabisa,” alieleza Dk Dkhary.
Alisema madaktari wanaofanya upasuaji huo ni madaktari bingwa wa upasuaji wa watoto (Pediatric Surgeon) au madaktari bingwa wa upasuaj wa njia ya mkojo (Urologist Surgeon) na kama kuna kesi ngumu wanaweza kusaidiana lakini upasuaji huo ni wa kawaida kabisa. Daktari huyo alisema watoto ambao wanazaliwa wakiwa na maumbile hayo ni vigumu kuelewa jinsia yake kwa kumtazama kwa macho katika sehemu zake za siri kwani wanakuwa na viungo vya jinsia ya kike na pia ya kiume.
“Watoto hawa kwa mzazi hata mzalishaji inakuwa ni vigumu kutambua kwa kuangalia kwa sababu ukimuangalia mtoto sehemu zake za siri anakuwa na kiungo cha kiume na pia maumbile ya kike na kwa chini anakuwa na tundu la kukojolea,” alieleza. Anasema katika hospitali hiyo wanapokea watoto waliozaliwa katika hali hiyo wengi ambapo karibu kila wiki wanawafanyia upasuaji wa kurekebisha maumbile baada ya kuwafanyia vipimo mbalimbali na kubaini jinsi yake.
“Kama ni mtoto wa kike utamfanya awe wa kike kwa kurekebisha maumbile yake, na kama ni wa kiume hivyo hivyo, na ni lazima kufanya vipimo kadhaa kwanza ili kuhakikisha jinsi ya mtoto,” alisema na kuongeza kuwa hakuna sababu maalumu inayoweza kusababisha kupata mtoto mwenye tatizo hilo.
Alitaja vipimo hivyo kuwa ni pamoja na vya damu kujua vinasaba vya mtoto na pia kuchukua kijinyama kwenye mdomo wa mtoto kupima baada ya kuiotesha pamoja na kipimo cha MRI kuona viungo vya ndani vya mtoto ni vya jinsi gani.
Chapisha Maoni