Image result for VIONGOZI WA MADHEHEBU
VIONGOZI wa kada mbalimbali wamesikitika namna rasilimali za Watanzania zinavyochotwa na kunufaisha mataifa ya nje, huku Watanzania wenyewe wakizidi kuzama katika dimbwi la umaskini.
Kutokana na hali hiyo, viongozi hao wa kidini, kiserikali na kisiasa katika mazungumzo na Gazeti hili kwa nyakati tofauti kuhusu ripoti ya Kamati maalumu ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi iliyoundwa hivi karibuni na Rais John Magufuli ikiongozwa na Profesa Nehemiah Osoro. Walisema jana kuwa sasa ukweli umebainika zaidi hivyo, jamii haipaswi kuwachekea wasaliti na badala yake, imuunge mkono kwa dhati Rais Mafuguli ili Watanzania washinde katika vita hii mbaya ya kiuchumi.
Mwenyekiti wa chama cha siasa cha Tanzania Labour Party (TLP) Augustine Mrema, alisema baadhi ya wabunge waliombeza Rais kuhusu sakata hili wanazidi kuumbuka namna walivyo wasaliti na wanaochezea akili za Watanzania. “Hao wabunge waache tabia ya kumsengenya Rais anapofanya jambo jema kwa Watanzania. Huo ni unaa wa kuwafanya Watanzania kama hawana akili wakati wana akili. Wapuuze. Wamuunge mkono Rais wetu anafanya mambo mazuri na makubwa. Watuachie Rais wetu tuliyemchagua na tunaona kumbe ndiye anayezidi kutufaa, anatuhurumia na kututetea,” alisema Mrema.
Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha Democratic Party (DP) John Cheyo (Mzee Mapesa) alisema, “Inaumiza sana maana kila mmoja ameona hata hisia za Rais. Ameonekana kuguswa na kuumizwa na namna Watanzania tunavyoibiwa na kudhulumiwa kwa mchango hata wa Watanzania wenzetu tuliowaamini.” “Nakubaliana naye kabisa katika vita hii lazima tupigane pamoja bila usaliti; pasiwe na advocate (wakili) mwanasiasa wa kutetea wezi maana unaona kamati zote mbili zimeonesha wazi kabisa tumeibiwa sana. Tuombe Mungu, tushirikiane tutashinda katika vita,” alisema Cheyo.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Raymond Saba alisema Watanzania bila kujali kabila, dini wala itikadi za kisiasa hawana budi kuungana kulinda rasilimali za taifa na kuzitumia kwa manufaa ya umma huku kila mmoja akizingatia uzalendo na uwajibikaji. “Rais asitetereke wala kutikiswa; tunazidi kumuombea maana anajua anachokifanya na walio makini wanaona kabisa namna alivyoamua kutumikia taifa hili kwa dhati… Watanzania wanafurahi kwa kazi hii,” alisema Padre Saba.
Naye Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakary Zubeir aliipongeza ripoti ya kamati iliyowasilishwa kwa Rais akisema imetunza uzalendo na ukweli na kwamba, italisaidia taifa. “Ripoti hii ikifanyiwa kazi sawasawa, itaondoa umaskini nchini. Watanzania sasa tujitambue, tubadilike na tuuvae upendo kwa kuheshimu mapenzi ya Mungu ili tutumike kwa manufaa ya umma,” alisema Mufti. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema, “Rais amepambana kwa ajili ya Watanzania, turudishe fadhila kwa kumuunga mkono.
Tuwakatae na kuwasuta wale ambao kazi yao ni kubeza na kushabikia hata wasiyoyajua au ili kupotosha umma kwa manufaa yao binafsi.” “Kosa kubwa wanalolifanya ni pale kila kitu wanapotaka kuingiza siasa; wanashindwa kukubali ukweli kuwa maendeleo au ubora wa huduma za kijamii kama shule, afya, barabara na maji huwa hazitolewi kwa kuangalia au kuuliza chama cha mtu; tunafaidika wote. Tumshukuru Rais, tumpongeze na tumuunge mkono,” alisema Lukuvi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation Joseph Butiku, alisema alipopewa nafasi na Rais kuzungumza kwa niaba ya wazee ndani ya ukumbi kuwa, vita ya uchumi ni vita kubwa na ngumu kuliko vita ya ukombozi wa silaha kama ziliyopigana nchi za Afrika katika kutafuta uhuru. “Sasa sisi wazee hata tuliosoma sawa, lakini hatuna ujasiri sasa tushukuru tumempata msomi jasiri mmoja; Rais John Magufuli… Watanzania niwaombe tumuunge mkono Rais.

Huwezi kwenda vitani kuzuia watu wasiwaibie au kuwanyang’anya walichowaibia, kisha mkagawanyika na mkategemea kushinda; hamuwezi kushinda.” “Sisi tuko pamoja hata hizi taasisi za kiraia zipo nyingi, naomba zikuunge mkono Watanzania tupate ushindi katika vita hii,” alisema Butiku.
KWAMATANGAZO YA BIASHARA KWAYA NYIMBO AINA ZOTE HABARI YEYOTE TUPIGIE   SASA KWA NUMBE,WHATSAPP FB //0623372368=0768163863
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top