Image result for sport pesa
MICHUANO ijayo ya Kombe la Sport Pesa Super Cup, mwaka 2018, inatarajiwa kufanyika Kenya ikishirikisha timu nane za Kenya na Tanzania.
Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Sport Pesa inayodhamini michuano hiyo, Abbas Tarimba alisema jana wamefurahishwa na ushindani ulioonyeshwa na timu katika michuano ya mwaka huu iliyomalizika juzi kwa Gor Mahia ya Kenya kutwaa ubingwa huo. Alisema pamoja na changamoto zilizojitokeza kwenye michuano hiyo, lengo lao la kuzinoa klabu kujiimarisha na ligi zao limefanikiwa na wanafurahi kuona hakuna malalamiko ya timu. “Tunafurahia hamasa na ushindani uliokuwepo kipindi chote cha michuano.
Kwa ujumla mambo yalienda vizuri na tumefanikiwa katika malengo yetu. Ombi langu kwa timu zilizofanya vibaya hasa zaTanzania kujipanga ili mwakani ziweze kufanya vizuri Kenya,” alisema Tarimba. Kocha Mkuu wa Gor Mahia, Zedekiah Otieno, alisema siri ya kikosi chake kutwaa taji hilo ni ubora na kutotegemea baadhi ya wachezaji. Otieno alisema walikuja na malengo na kucheza kwa misingi waliyojipangia ndiyo maana wakafanikiwa kile walichokusudia.
“Nimefurahi kuona tunatwaa ubingwa huu kwa rekodi ya pekee ya kushinda mechi zote tatu ndani ya muda wa kawaida wa dakika 90. Lakini pia tumecheza bila wachezaji wetu saba ambao wapo kwenye timu zao za taifa. Tunashangaa kuona timu za Tanzania zinasingizia hazikuwa na wachezaji wao muhimu,” alisema Otieno. Kocha wa AFC Leopards, Dennis Kitambi alisema walipoteza mchezo wa fainali kwa sababu hawakucheza kwenye kiwango chao cha kila siku tangu walipoanza michuano hiyo.
Kitambi raia wa Tanzania alisema wachezaji wake walicheza vizuri kwa dakika 20 baada ya hapo waliwapa Gor Mahia, nafasi ya kutawala. Hata hivyo, alijisifu kwa kupambana na kwenda mapumziko wakiwa hawajaruhusu bao. “Kipindi cha pili hali ilizidi kuwa mbaya baada ya kufungwa bao la kwanza. Nilibadilisha mfumo lakini wenzetu walikuwa bora zaidi. Tunakubali matokeo na kujipanga kulipa kisasi kwenye Ligi Kuu ya Kenya,” alisema Kitambi.
Kwa kutwaa ubingwa, Gor Mahia ilipata zawadi ya dola 30,000 (Sh milioni 66) na kombe wakati mshindi wa pili, AFC Leopards, aliambulia dola 10,000 za Marekani sawa na Sh milioni 22. Michuano hiyo ilizishirikisha pia Nakuru All Stars ya Kenya iliyotolewa na Gor Mahia kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili.
Wawakilishi wa Tanzania walikuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom, Yanga waliotolewa na AFC Leopards kwenye nusu fainali na kuishia kupata zawadi ya dola 5,000 kama zawadi zao. Wengine ni Simba, Singida United na Jangombe Boys ya Zanzibar zilizotolewa hatua ya awali tu. Mshindi, Gor Mahia atachuana na timu ya Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England, Julai 13 mwaka huu uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
KWAMATANGAZO YA BIASHARA KWAYA NYIMBO AINA ZOTE HABARI YEYOTE TUPIGIE   SASA KWA NUMBE,WHATSAPP FB //0623372368=0768163863
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top