UMOJA wa Mataifa (UN) umefunza zaidi ya vijana 20,000 kuhusu malengo ya maendeleo endelevu ya dunia na hadi mwishoni wa mwaka huu watafikia 50,000.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Mashirika ya UN, Alvaro Rodriguez wakati akifungua kambi ya TIMUN 2017 mjini hapa. Alisema mafunzo hayo yaliyofanywa kwa njia mbalimbali ikiwamo kampeni ya kuhamasisha uelewa yanakwenda vizuri tangu yalipozinduliwa Juni mwaka jana. Lengo la mafunzo hayo ni kuhamasisha vijana zaidi washiriki kufanikisha malengo 17 ya maendeleo endelevu duniani.
Akizungumza katika hafla ya kambi ya mwaka huu ya Tanzania International Model United Nations (TIMUN), Chuo Kikuu cha Nelson Mandela mjini Arusha, Rodriguez alielezea kufurahishwa na idadi hiyo kubwa ya vijana waliohamasishwa na kusema malengo ya maendeleo endelevu 2030 yanamhitaji kila mmoja kushiriki. Alielezea umuhimu wa ushiriki wa vijana katika maendeleo kutokana na uwingi wao nchini.
Asilimia 67 ya watu nchini ni vijana. Rodriguez alishukuru machampioni kwa kuwezesha vijana wenzao kutambua malengo endelevu ya dunia na kuwataka kuendelea kufanya vizuri zaidi katika kuwashawishi vijana wenzao kuelewa na kushiriki katika malengo hayo endelevu. “Nataka kuwatafadhalisha kwamba huu ni mwanzo tu, kuna mengi ya kufanya.
Kama Umoja wa Mataifa, tunawataka wote mshiriki, si tu katika kuelimisha kuhusu malengo haya ya dunia, lakini pia katika kuangalia mwenendo wa maendeleo hayo katika jamii na yanavyotekelezwa. Tukio hili la TIMUN linasaidia kuongeza uwezo wa kufikia malengo ya dunia,” alisema. Vijana 50 wa kwanza machampioni walifunzwa mwaka jana TIMUN 2016.
Kwa sasa vijana machampioni 500 nchini wanapeleka ujumbe kwa vijana 20,000. Ujumbe ambao umekuwa ukisambazwa na machampioni kwa wenzao ni: “Kama watu hawatajua malengo ya maendeleo endelevu, hawataweza kufanya malengo hayo kuwa ya kweli,” alisema Gloria Nassary, mmoja wa vijana 50 waliopewa mafunzo ya kwanza ya kuwa machampioni. /IMEANDIKWA MWANDISHI WA ARUSHA






Chapisha Maoni