HALMASHAURI ya Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora imewafukuza kazi watumishi watano baada ya Baraza la Madiwani kuridhia.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Revocatus Kuuli jana aliwataja watumishi waliofukuzwa kuwa ni Daudi Magembe (mlinzi) na Nasibu Ngoitanile (tabibu msaidizi). Aliwaambia waandishi wa habari kuwa, watumishi wengine ni Revocatus Msaku (ofisa mtendaji wa kijiji), Emmanuel Andrew (ofisa mtendaji kata) na Kizito William (dereva).
Kuuli alisema watumishi hao walifukuzwa kazi Mei 12 mwaka huu kwa makosa mbalimbali ya wizi wa fedha, utoro, na ulevi na kuisababishia halmashauri hasara. Alisema pamoja na kuwaonya watumishi hao hawakubadilika jambo lililofanya madiwani wakatae kuendelea nao kazini.
Kuuli aliwataka watumishi wanaofanya kazi kwa mazoea kuacha mara moja kwani atakayeshindwa kuhimili kasi, ataondolewa. Baadhi ya waliofukuzwa kazi walisema uamuzi uliofanywa na madiwani hawawezi kuupinga hivyo watatafuta kazi nyingine za kufanya ili waweze kutunza familia zao.
                  IMEANDIKWA NA LUKAS RAPHAELI TABORA
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top