Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi. Eda Sanga
Tamwa) kimesisitiza kuwa kuwafukuza wasichana wanaopata mimba shuleni ni kuwanyima haki yao ya kupata elimu.
Kimesema hatua hiyo ni sawa na kuwafungia milango ya maendeleo wakati elimu ndio njia ya kuwatoa katika umaskini. Tamwa imesema hayo baada ya wabunge, hususan wabunge wanawake kutaka wasichana kufukuzwa shule pindi wanapopewa mimba kukomesha tatizo hilo.
Wabunge walitoa msimamo huo wakati wa kujadili hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma.
Taarifa ya Tamwa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilieleza mazingira ya shule wanakosoma wasichana hao siyo rafiki kwa wanafunzi wa kike na makundi rika ambayo husababisha watoto pia kufundishana na kushiriki katika matendo ya ngono zembe. Ilisema matokeo ya matendo hayo ni mimba, Ukimwi na magonjwa ya zinaa.
‘’Tamwa ingetarajia wabunge wote, lakini hasa wanawake, kuelewa vizuri mazingira yanayofanya wasichana kupewa mimba kwani wengi ni wanaotoka familia masikini vijijini na mijini,’’ ilisema taarifa hiyo. Pia iliongeza kuwa katika umasikini wao ni rahisi kunaswa kwa kurubuniwa na wanaume wenye pesa, magari na ahadi za kuwasaidia kutoka katika umasikini huo.
Ilisema bila malezi mema na uangalizi mzuri, wa karibu wa watoto hasa wasichana kutoka kwa wazazi au walezi wao, watoto watakuwa wahanga kwa jamii isiyowajali. Tamwa ilisema matangazo ya kibiashara katika redio, runinga na intaneti yamejikita katika kutukuza ngono, urembo na kila aina ya starehe huku mitandao ya kijamii ikichukua muda mwingi wa vijana siku hizi.
Ilieleza masuala hayo huchangia katika kuwatamanisha na kuwafanya wasichana waige tabia za ulimwengu wa utandawazi kinyume na utamaduni wao na maadili. Tamwa ilisema vyombo hivyo vingine si vya serikali lakini vipo katika mfumo halali wa biashara baada ya kupewa leseni na serikali. ‘’Badala ya kuwafukuza wasichana hao, ingekuwa wajibu wa serikali kuwatetea kwa sababu chanzo cha tatizo hili ni udanganyifu, ubabe wa wanaume na udhaifu wa vijana wadogo,’’ilisema Tamwa.
Tamwa ilisema dhana kuwa wanaopata mimba shuleni wasiruhusiwe kuendelea kwa kuwa wamejifukuzisha na ya kuwaruhusu kuendelea na shule wakijifungua ni kuongeza mimba mashuleni haina ukweli. Ilisema dhana hizo zingekuwa na ukweli tatizo lisingekuwapo na tabu wanazopata wasichana wanaoachishwa shule zingekuwa onyo kwa wengine kutoshiriki ngono tena.






Chapisha Maoni