SIMBA ya jijini Dar es Salaam na Mbao FC ya Mwanza zinakwaana leo katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho au FA Cup, katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. Ni mpambano wa vigogo wa soka pamoja na timu iliyosurika kushuka daraja katika Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika Jumamosi iliyopita.
Hata hivyo, pamoja na Mbao kunusurika kushuka daraja, lakini timu hiyo imedhihirisha uimara wake pale ilipoifunga mara mbili Yanga na nusura iifunge Simba kama sio wekundu hao wa Msimbazi kuchomoa katika dakika za mwisho.
Kimsimamo, Simba imemaliza ikiwa ya pili wakati Mbao FC ilimaliza ligi hiyo kuu ikiwa katika nafasi ya 12, hivyo ukiangalia kwa haraka utaona kama timu hizo ziko katika madaraja tofauti.
Pamoja na Mbao kumaliza katika nafasi hiyo lakini bado timu hiyo iko vizuri na inaweza kufanya lolote ambalo halitarajiwi na wadau wengi wa soka, hivyo kinachotakiwa ni mchezo huo uchezeshwe kwa haki ili bingwa halali apatikane.
Ligi iliyomalizika ilikuwa na changamoto nyingi zilizosababisha malalamiko kibao kutoka kwa timu shiriki, hivyo ni jukumu la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha mchezo wa leo unatoa bingwa wa ukweli.
Baada ya Yanga kupata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika kufuatia kuwa mabingwa wa Bara, mpambano wa leo ndio utatoa mwakilishi mwingine wa kimataifa.
Bingwa wa Kombe la FA ndiye atakayewakilisha taifa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika, mashindano ambayo ni ya pili kwa ukubwa kwa klabu barani. Tunasema kuwa tunahitaji bingwa wa ukweli katika fainali hiyo, ambayo inatarajia kushuhudiwa na watazamaji wengi wakiwemo Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao wako Dodoma katika Bunge la Bajeti.
Wadau wa michezo wamechoka kuona wawakilishi wetu wa nchi wakifanya vibaya kila wanaloshiriki katika mashindano ya kimataifa na hii inatokana na kutokuwa na mashindano yenye nguvu ya kutafuta wawakilishi wetu.
Ni matumaini yetu kuwa, mchezo wa leo utatoa burudani safi kwa wapenzi watakaofika kwenye Uwanja wa Jamhuri na wale watakaokaa mbele ya luninga zao wakiushuhudia wakati bingwa wa Kombe la FA akisakwa.
Mbao pamoja na ugeni wake na kucheza Ligi Kuu kwa ‘bahati’ ni timu iliyoonesha mchezo safi na kufanikiwa mara mbili kuifunga Yanga katika mchezo wa nusu fainali ya FA na mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu.
Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ni huru kwa timu zote, kwani Simba kwao ni Dar es Salaam na Mbao ni Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, hivyo kila mmoja atakuwa na nafasi ya kuonesha uwezo wake.
Pamoja na Simba kutarajia kuwa na mashabiki wengi, lakini Mbao nao watafaidika kupata sapoti kutoka kwa mashabiki wa Yanga, ambao ni wapinzani wakubwa wa Simba. Yote ni yote, mashabiki wanataka bingwa wa ukweli katika mchezo wa leo.
Chapisha Maoni