MKAZI wa Mtaa wa Kanyerere uliopo katika Kata ya Mahina, Wilaya ya Nyamagana jijini hapa, Maximillian Ndegere (40) amejiua muda mfupi baada ya kumjeruhi kwa risasi mkewe, Teddy Patrick (38) aliyepigwa risasi mgongoni na kutokea tumboni.
Teddy naye aliaga dunia jana. Ndegere alijeruhi na kujiua kwa kujipiga risasi kifuani na mkono wa kushoto kwa kutumia bastola yenye namba za usajili BJ 306666 CAR Na. 00103129.
Akizungumza jana jijini hapa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema tukio hilo lilitokea Mei 25 mwaka huu majira ya saa 4.15 usiku. Katika tukio hilo, alisema baada ya mkewe kujeruhiwa alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jambo ambalo alisema ni kosa kisheria kwa sababu ya kutopata barua ya Polisi ya PF 3.
Alisema wawili hao inasemekana walikuwa ni wafanyabiashara wa samaki na mwanaume alikuwa anamiliki silaha yake kisheria na kwa muda ambapo mauaji yalipofanyika walikuwa wametoka kwenye biashara zao wakiwa hawana ugomvi wowote.
Alisema baada ya kuwasili nyumbani, wakiwa chumbani kwao ilisikika milio ya risasi hali iliyowafanya majirani na watu wa karibu kuingia ndani kwa lengo la kuwanusuru na ugomvi wao, lakini walimkuta Teddy akipiga yowe huku akiwa amejeruhiwa kwa risasi akiomba msaada huku mumewe akiwa tayari amekufa kwa kujipiga na risasi.
“Wananchi walitoa taarifa Polisi kuhusiana na tukio hilo, na ndipo walipofika kwenye eneo la tukio na kumkimbiza Teddy hospitalini kupatiwa matibabu, lakini leo (jana) Mei 26 majira ya saa 3.30 asubuhi alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu,” alifafanua Msangi.
Alisema chanzo cha mauaji hayo bado kinachunguzwa na kwamba jeshi la polisi linaendelea na upelelezi kuhusiana na mauaji hayo na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando na uchunguzi ukikamilika itakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top