WACHEZAJI wa klabu ya soka ya Simba wameahidiwa mamilioni ya fedha endapo leo wataibuka na ushindi dhidi ya Mbao FC ya Mwanza, katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA.
Mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, ambapo mshindi mbali na kutwaa taji hilo, pia atapata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika. Pia mshindi huyo atakabidhiwa kitita cha Sh milioni 50.
Homa na presha kwa mashabiki na viongozi mbalimbali wa timu hizo imekuwa kubwa na wengi wao tayari wametoa ahadi mbalimbali kwa lengo la kuwapa hamasa wapambanaji wao kuweza kushinda mchezo huo na kupaa nafasi hiyo ya kuungana na Yanga ili kubeba bendera ya taifa kwenye michuano ya kimataifa.
AHADI KWA WACHEZAJI Wabunge mbalimbali ambao ni mashabiki wa timu ya Simba wametoa ahadi ya Sh milioni 20 endapo timu yao itaifunga Mbao na kutwaa taji hilo kama ambavyo wamekusudia.
Mbali na wabunge nao, viongozi wa timu hiyo wameahidi kutoa asilimia kubwa ya fedha za zawadi kwa wachezaji wao endapo watafanikiwa kutwaa taji hilo na kupata nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa.
Simba ndiyo wenyeji katika mchezo huo wa leo na tayari wamewasili Dodoma tangu juzi saa 12 za jioni wakitokea Morogoro, ambako waliweka kambi ya muda kujiandaa na mchezo huo pekee kwao katika kurudi kwenye michuano ya kimataifa baada ya kuikosa kwa muda mrefu.
Kocha wa Simba amesema huo ni mchezo muhimu kwao na ni lazima wacheze kwa nguvu ili kuhakikisha wanapata ushindi utakaowafanya kutimiza kile walichokikusudia ambacho ni kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Mcameroon huyo alisema anatambua kuwa mchezo utakuwa mgumu, lakini wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata ushindi kwa sababu wamewasoma vya kutosha wapinzani wao na hakuna shaka kwamba mambo yatakuwa mazuri.
“Mbao ni timu nzuri lakini katika mchezo wa kesho (leo) watatusamahe kwani tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda na kuirudisha hadhi ya Simba, lengo ni kushiriki michuano ya kimataifa na ni lazima litimie,” alisema Omog.
Kocha huyo alisema kikosi chake hakina mchezaji majeruhi, hivyo anaamini mipango yake itakwenda sawa na kumaliza mchezo huo mapema ili kutwaa taji hilo ambalo msimu uliopita walilikosa baada ya kutolewa hatua ya robo fainali na Coastal Union.
Mbao, timu ambayo inapewa sapoti kubwa na mashabiki wa Yanga ndiyo ya kwanza kuwasili Dodoma siku nne na kufanya mazoezi ya kutosha kwenye uwanja wa Jumhuri. Timu hiyo inayofundishwa na kocha Etienne Ndyariagije, imekuwa na matumaini makubwa ya kufanya maajabu mengine leo kwa kuifunga Simba na kutwaa taji hilo.
Kuelekea mchezo huo nao kama ilivyo kwa Simba tayari wamepoka ahadi mbalimbali kutoka kwa viongozi na wakazi wa Mwanza kuwa endapo watashinda. Mmoja anayeongoza kampeni za Mbao ni Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongela ameahidi kuwapa basi kubwa la kusafiria timu hiyo endapo wataifunga Simba na kutwaa ubingwa wa Kombe la FA.
Pia kiongozi huyo alisema wakazi wa Mwanza wamechanga kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili yao hivyo wanapaswa kucheza kwa nguvu ili kuhakikisha wanatwaa taji hilo. “Mnatakiwa kucheza kwa nguvu na kuipigania timu yenu msiogope majina nyie na wachezaji wa Simba hamna tofauti tena pengine nyie mna uwezo mkubwa sema hamjapata bahati ya kusajiliwa huko ila hiyo ndiyo nafasi pekee kujitangaza,” alisema Mongela.
Kocha wa Mbao alisema mchezo wa fainali utakuwa mzuri na wamejipanga kumaliza shughuli hiyo mapema kutokana na maandalizi waliyofanya kuelekea mchezo huo. Kocha huyo alisema pamoja na kwamba atamkosa mshambuliaji wake tegemezi Bernad Mujweaki anayesumbuliwa na maumivu ya nyama za paja, ana imani na washambuliaji waliopo fiti kuelekea mpambano huo wa leo.
“Tunaiheshimu Simba ni timu kubwa ukilinganisha na sisi Mbao, wanatuudhi kwa mambo mengi hata wachezaji wangu wengi hapa wanatamani kuichezea timu hiyo, lakini tumejipanga lengo letu likiwa ni ushindi ili kuhitimisha kazi tuliyoianza huko nyuma,” alisema Ndyariagije.
Mchezo huo unatarajiwa kuanza majira ya saa 10 za jioni hapa Dodoma na endapo hadi dakika 90 mshindi atakuwa hajapatikana mchezo huo utaongezwa dakika 30 na kama pia hakutakuwa na timu iliyopata ushindi utaamuliwa na mikwaju ya penati. Wachezaji
Chapisha Maoni