MCHEZO wa leo presha tupu! Ni fainali za Kombe la Shirikisho la Azam (FA) kati ya Simba dhidi ya Mbao FC. Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, ukitarajiwa kuteka hisia za mashabiki wengi wa soka hasa kutokana na ushindani wa timu hizo kwenye mechi walizokutana.
Ni mchezo muhimu kwa kila timu. Wekundu wa Msimbazi Simba wakitaka kushinda ili kushiriki michuano ya kimataifa baada ya kukosekana kwa karibu miaka mitano. Simba inalazimika kupambana kufa kupona ipate nafasi hiyo, hasa baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu uliokwenda mtaa wa pili, Yanga.
Aidha, Mbao FC wababe wa vigogo sio timu ya mchezo wala kuidharau hasa baada ya kuzikazia timu zenye majina makubwa na hasa kwa Yanga ambao walifungwa michezo miwili, mmoja wa ligi na mwingine wa nusu fainali FA. Mbao imekuwa na jeuri zaidi inapokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, CCM Kirumba Mwanza, hupambana kwa kila njia ilimradi kupata matokeo mazuri na kuwapa raha mashabiki wake. Lakini inapotoka nje ya uwanja wake jeuri yote kwisha, nafasi yao ya ushindi ni ndogo.
Ingawa hilo halipaswi kuangaliwa kwa asilimia kubwa kwa sababu mara nyingi matokeo ya mpira huwa hayatabiriki. Matokeo hupatikana uwanjani tu na kila mmoja ana nafasi ya kuwa bingwa katika uwanja huo ambao sio wa Simba wala wa Mbao. Timu hiyo ya jijini Mwanza baada ya kunusurika kushuka daraja inataka kuweka historia nyingine mpya ya kushiriki michuano ya Kimataifa mwakani.
Inataka kuwa timu ya Kanda ya ziwa kuwakilisha nchi kimataifa hasa baada ya miaka mingi kutokuwa na timu yoyote nje ya Dar es Salaam inayofanya vizuri na kushiriki michuano nje ya Tanzania baada ya Mtibwa na Prisons kufanya hivyo miaka zaidi ya 10 iliyopita. Kwa muda mrefu sasa timu ambazo zimekuwa zikiwakilisha nchi kimataifa zinatoka Dar es Salaam ambazo ni Yanga, Azam na Simba na hupokezana vijiti kutegemea na jinsi zilivyofanya vizuri kwenye michuano ya ligi.
Sio Simba wala Mbao kila mmoja anataka kuweka historia yake ya kushinda na kusonga mbele. Timu hizo zitakutana kwa mara ya tatu leo. Mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, Simba ikishinda bao 1-0 kwenye Ligi Kuu kabla ya kuibuka tena na ushindi wa mabao 3-2 kwenye uwanja wa CCM Kirumba katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu. Hata hivyo pamoja na ushindi huo, wachezaji wa Simba ‘walilala na viatu’ siku hiyo kutokana na soka waliyopigiwa na Mbao.
Mbao ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 mpaka dakika ya 86, kabla Simba haijabadili matokeo na kupata mabao matatu katika dakika za mwisho za mchezo huo. Hivyo, ni lazima Simba itaingia kwa tahadhari kubwa ikijua wazi kuwa inacheza na timu ya aina gani baada ya kuzisumbua ya Mbao kuwa sumbufu kwa Yanga na Mtibwa. Mtibwa iliwahi kufungwa mabao 6-2 kwenye uwanja wa CCM, Kirumba. Ni matokeo ambayo yalizishtua timu nyingi na hata mashabiki wa soka.
Lakini kwa kuwa tayari Simba na Mbao zinafahamiana na kila mmoja amejifunza kitu kulingana na matokeo yaliyopita, kazi itakuwa ni kubwa uwanjani na hakuna shaka mashabiki wa soka wanatarajia kupata burudani safi. Katika kuhakikisha Simba inachukua ubingwa wa FA imefanya maandalizi yake Morogoro kwenye mazingira tulivu. Ni sehemu ambako wanaamini wakitoka ni lazima wafanye vizuri mechi iliyo mbele yao.
Tangu kuanza kwa msimu uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita, timu hiyo imekuwa ikitumia Morogoro kwa maandalizi yake ya michuano mbalimbali. Kocha Msaidizi wa Simba Jackson Mayanja anasema mchezo huo wanahitaji matokeo na kuchukua ubingwa na kwamba walihitaji mazingira yaliyotulia kama Morogoro kuwaandaa wachezaji kisaikolojia.
“Tunashukuru uongozi kwa kuwa nasi bega kwa bega kuhakikisha kwamba tunashinda mchezo wetu dhidi ya Mbao. Tunaijua Mbao FC ni wazuri na hatuwezi kuwabeza, tumejipanga vizuri,” anasema. Mayanja anasema kikosi chake kiko tayari kwa mapambano, lengo lao ni kuhakikisha wanashinda na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Simba inawategemea nyota wake akiwemo Laudit Mavugo, mchezaji aliyepata tuzo ya bao bora la msimu wa Ligi Kuu 2016/2017 Shiza Kichuya, Ibrahim Ajibu, Mohamed Ibrahim, Janvier Bukungu, Abdi Banda, Juuko Murshid, Mchezaji bora wa Ligi Kuu 2016/2017 Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jnr’, Daniel Agyei na Mzamiru Yasini. Nyota hao wamekuwa wakiibeba timu hiyo kwa nyakati tofauti na kila mmoja ana umuhimu wake kulingana na anavyopewa nafasi na benchi la ufundi.
Kocha wa Mbao FC, Ettiene Ndayiragije ni aina ya mwalimu anayetaka kuleta mapinduzi. Anajitahidi kukiongoza kikosi chake kwenye mafanikio. Mbao ina kikosi kizuri kinachojituma kikiongozwa na Boniphace Maganga ambaye aliwahi kuichezea Simba. Pia, kuna Jamal Mwambeleko, David Mwasa, Asante Kwasi, Yussuf Ndikumana, Ibrahim Njohole, Salmini Hoza, George Sangija na Habibu Haji na Pius Buswita.
Wachezaji ambao wamekuwa bora na kutajwa na timu mbalimbali kwenye usajili ujao ni Ndikumana na Kwasi ni wachezaji wa kigeni kutoka Burundi na Ghana ambao wameonekana wakifanya vizuri. Akizungumzia mchezo huo, Ndayiragije anasema wako vizuri na tayari kwa mchezo huo. “Tunahitaji kuweka historia ya ubingwa wa FA na kushiriki michuano ya kimataifa.
Huu ni mchezo muhimu zaidi kwa kupata matokea na ushindi,”anasema. Anasema aihofii Simba na kwamba anaichukulia kama timu nyingine alizowahi kukutana nazo. Mashabiki wa soka nchini wamekuwa wakiipa nafasi kubwa Simba na wengine wakisema Mbao FC ndio watakaokuwa mabingwa. Mchezo unatabiriwa kuwa mgumu na yeyote anaweza kushinda na kuchukua ubingwa.
Itakumbukwa kuwa kabla ya Simba na Mbao kufika fainali kwenye michuano hiyo, zilianza zaidi ya timu 30 za madaraja ya chini, zikaingia ligi daraja la pili, daraja la kwanza na Ligi Kuu na mwisho wa siku hizo ni timu mbili bora. Pia, itakumbukwa kuwa fainali ya msimu uliopita ilizikutanisha Yanga dhidi ya Azam FC katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga ikachukua ushindi.
Msimu huu timu hizo zilitolewa mapema kwenye hatua ya nusu fainali na leo ni timu nyingine mpya yaani Simba na Mbao zinazotarajiwa kuweka historia nyingine. Hivyo, kwa kuwa tayari Yanga imejihakikishia nafasi nyingine ya kimataifa baada ya kutwaa ubingwa wa ligi basi anayesubiriwa ni kati ya Simba na Mbao kuungana na Yanga kwenye michuano ya kimataifa mwakani. Kila la heri Simba na Mbao!
KWAMATANGAZO NYIMBO TUPIGIE 0623372368
Chapisha Maoni