HIVI majuzi kikosi cha wachezaji wa timu ya taifa ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka ya 17, Serengeti Boys kilirejea nchini baada ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa U-17.
Timu hiyo ambayo ilianza vema michuano hiyo ilitolewa baada ya kufungwa na Niger, 1-0 kwenye mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi. Lakini ilitolewa huku ikiwa imeshatoa sare na Mali na kuifunga Angola, hali ambayo imeashiria kuwa ilikuwa imejitahidi kwa kiwango chake.
Kutolewa kwa timu hiyo kumepokewa kwa mitazamno tofauti katika jamii ambapo wapo waliobeza lakini kwa kiasi kikubwa wadau wa soka wengi wameipongeza timu hiyo kwa kile walichosema kuwa imejitaidi lakini bahati haikuwa upande wao.
Kwa upande wake Waziri mwenye dhamana ya michezo ambae ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akiwapokea wachezaji hao alisema kuwa ni washindi ambao wameifuta machozi Tanzania ya miaka 37.
Binafsi ninaungana na Waziri wangu huyo katika kuwatia moyo wachezaji hao kwa kile ambacho wamekifanya kuwa ni kikubwa na faraja kwa Tanzania. Mara ya mwisho kwa timu ya Tanzania kushiriki michuano hiyo ilikuwa ni mwaka 1979 ambapo ni timu ya wakubwa ndio iliwakilisha nchi kwenye michuano hiyo.
Lakini tangu hapo hatukuwahi kushiriki kwenye fainali hizo hadi mwaka huu ambapo vijana hao wa U-17 walivyofanikiwa kuiwakilisha nchi. Hii inamaanisha kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa vijana hawa kuiwakilisha tena nchi kwenye michuano ya U-20 ambayo wanaweza kufanya vema zaidi.
Kwa kuwa kwa sasa ni mwakani tu watakuwa wakichukuliwa sio U-17 na badala yake watakuwa ni U-20 wakifahamika kama Ngorongoro Heroes ni wakati sasa wa kuandaliwa. Kama wameweza kufikia hatua hiyo kwa mwaka huu wakiwa U -17 ni dhahiri kuwa wakiwa U-20 wanaweza kutumia uzoefu walioupata kwenye U-17 kufanya makubwa zaidi.
Hawa wanaweza kushinda michuano hiyo na kuiletea heshima kubwa nchi kwa kuwa wameshapata mwanga wakiwa bado wadogo, kilichobakia kwa sasa ni kuwandeleleza. Kwa kuwa Waziri Mwakyembe ameshaonesha nia hiyo ni wazi kuwa kwa sasa kinachotakiwa ni kuwaandaa mapema na hasa katika kuwatafutia michezo mingi zaidi ya kujifua.
Lakini pia kwa wale ambao kwa sasa ni wanaingia kuwa U-17 ambao wanachukua mikoba ya hawa kaka zao wanaoenda kuwa U-20 na wao waandaliwe kwa kuwa mwaka 2019 michuano yao itafanyikia hapa nchini.
Michuano hiyo kwa kuwa itafanyikia hapa nyumbani wachezaji hao wanaweza kufanya vema zaidi kwa kuwa watachezea kwenye viwanja walivyokwisha vizoea. Maandalizi yao yahusishe kuchukua vipaji kutokea kwenye michuano mbalimbali ya wachezaji wadogo ili waanze maandalizi kuanzia sasa ili waje kuwa wachezaji wakubwa wa baadaye.
KWAMATANGA
Chapisha Maoni