SERIKALI imepiga marufuku wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, wanaowazuia wananchi kuuza chakula cha ziada katika maeneo yenye upungufu, kuacha kufanya hivyo mara moja. Msimamo huo ulitolewa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba wakati akizungumza na vyombo vya habari mjini hapa jana.
Alisema wajibu wa viongozi hao ni kuwaelimisha wananchi ili wafanye tathmini, kuangalia wingi wa chakula walicho nacho na kuuza cha ziada katika maeneo yenye uhaba wa chakula katika maeneo mengine kama Dar es Salaam, ambayo hayana mashamba.
“Kutokana na kitendo hicho cha kuzuia wananchi hao kuuza chakula hicho ndani ya nchi kwenye maeneo yenye uhaba wa chakula, wanasababisha upungufu wa chakula usio wa lazima au usio na umuhimu,” alisema.
Alisema wakulima wanatakiwa kuchukua tahadhari ya kutouza chakula chote kutokana na ukweli kwamba nchi zinazoizunguka Tanzania, zina hali mbaya kutokana na ukame uliozikumba, kwani zikiachwa zinunue zinaweza kununua kiasi kikubwa na kuiacha nchini bila ya akiba ya kutosha.
Tizeba alisema, uuzaji holela wa chakula hautakiwi kutokana na ukweli kwamba hivi sasa bei ya chakula ipo chini, lakini miezi ya kiangaza bei ya chakula itakuwa kubwa. Akizungumzia kuhusu Maadhimisho ya Uhamasishaji wa Unywaji Maziwa kwa mwaka huu, Tizeba alisema kitaifa yatafanyika mkoani Kagera katika Viwanja vya Kyakailabwa.
Alisema maadhimisho hayo, yanayolenga kuongeza unywaji maziwa kutoka lita 47 hadi 200 kwa mwaka, yatatanguliwa na Wiki ya Uhamasishaji Maziwa kuanzia Mei 28 hadi Juni mosi ambayo ni siku ya kilele.
Tizeba alisema maadhimisho hayo yenye kaulimbinu ‘Kunywa Maziwa, Furahia Maisha,’ yanalenga kuelimisha wananchi juu ya matumizi ya maziwa, kama chakula bora kwa watu wa rika zote.
Akizungumzia shughuli zitakazoambatana na maadhimisho hayo yanayosimamiwa na Bodi ya Maziwa Tanzania, Waziri Tizeba alisema ni pamoja na maonesho ya bidhaa za maziwa na ugawaji wa maziwa kwa vituo vya wahitaji maalumu kama yatima, magereza, wazee na katika hospitali
KWAMATANGAZO YA BIASHARA TUPIGIE 0623372368
Chapisha Maoni