JANA Rais John Magufuli alipokea taarifa ya Kamati Maalumu aliyoiunda Machi 29, mwaka hu, kuchunguza mchanga ulio katika makontena yenye machanga wa madini (makinikia) yaliyopo maeneo mbalimbali nchini yaliyozuiliwa na Serikali kusafirishwa nje ya nchi.
Uchunguzi huu ulitokana na viwango vya madini kwenye makinikia hayo kutojulikana, na hata mikataba ya uchenjuaji makinikia nayo ikiwa haiwekwi wazi. Hali hii ilileta hisia wazi kuwa nchi inaibiwa na hainufaiki na uchimbaji wa madini.
Kama ilivyoelezwa katika habari ndani ya gazeti hili, Kamati imebaini kuwapo mchezo mchafu wa kuliibia taifa madini kwa kisingizio cha kusafirisha mchanga na hali hiyo, imechangia kuliweka taifa katika hali ya umasikini unaoonekana sasa.
Kamati hiyo ilikuwa na hadidu za rejea kadhaa zikiwa za uchunguza makinikia yaliyopo bandari ya Dar es Salaam, bandari kavu na migodini kwa kupekua na kubaini vitu vilivyomo ndani pamoja na kuchukua sampuli za makinikia ili kuzifanyia uchunguzi wa kimaabara ili kubainisha aina, kiasi na viwango vya madini yatakayoonekana katika makinikia kisha, kubainisha thamani ya madini hayo na kuchunguza utendaji wa Wakala wa Serikali wa Ukaguzi Madini (TMAA).
Kupitia uchunguzi huo, Kamati ilibaini kuwa thamani ya dhahabu katika makontena 277 yaliyozuiliwa bandarini ni kati ya Sh bilioni 676 na bilioni 1,147 za Kitanzania zilizokuwa zinatoka nje ya nchi na kuwaachia mashimo Watanzania.
Sisi tunampongeza Rais Magufuli kwa kuunda Kamati hiyo, kuiamini na kuheshimu mapendekezo yake kiasi cha kuyafanyia kazi mara moja na pia, tunaipongeza Kamati kwa kufanya kazi kijasiri, kiadilifu na kizalendo hata kutoa taarifa.
Kwa mara nyingine tunasema tunampongeza Rais kwa kuwa sio jambo lililozoeleka sana kwa Watanzania kwani ripoti nyingi za kamati au tume, matokeo yake yalikuwa yanaishia katika majalada ofisini.
Pamoja na pongezi hizo, tunaishauri Serikali kukaza uzi na kusambaza moto huo kwenda sekta mbalimbali ambazo sio siri, nyingine nazo zimechangia kukuza umasikini wa Watanzania kupitia wizi na uhujumu uchumi unaofanikishwa na Watanzania waliopewa dhamana na kuaminiwa na Watanzania wenzao kupitia serikali, eti kwa manufaa ya mataifa ya nje.
Ndiyo maana tunasema, kwa kadiri itakavyofaa, Rais na Serikali yake waangalie pia uwezekano wa kuunda kamati maalumu kushughulikia masuala yote tata katika sekta nyingine mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuhakikisha kwamba wanayofanya ni kwa ajili ya masilahi ya Watanzania wote na siyo wachache.
Kamati ya wataalamu ilitekeleza kwa ufanisi mkubwa jukumu la Makati hiyo ndiyo dira ya kamati tunazotaka ziundwe kuchunguza sekta zinaoonyesha utata wa mapato yetu na kuhujumu uchumi kwa makusudi kabisa na wale wenzetu wanaopewa jukumu la kuzisimamia sekta hizo. Hongera sana Serikali, hongera sana Watanzania kwa kubaini ufisadi huo uliokuwa unawanufaisha watu wachache.
KWAHABARI BIASHARA TUPIGIE 0623372368






Chapisha Maoni