SERIKALI haitarudi nyuma kupambana na watu wanaochafua sifa ya nchi kwa kuua watu wasio na hatia wilayani Kibiti, Pwani. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alitoa msimamo huo wa serikali bungeni jana baada ya Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) kuomba mwongozo Bunge lisitishe shughuli zake kujadili mauaji yanayotokea Kibiti, Pwani.
Selasini aliomba Bunge lisitishe shughuli zake na wabunge wote waungane na wa huko kutoa mawazo ya kuwapata wahalifu hao. Mwenyekiti wa Bunge, Idd Azzan Zungu alipokea mwongozo huo na kumpa nafasi Waziri Mwigulu kutoa ufafanuzi huo. Mwigulu alisema, serikali haikubali kuona Watanzania wanaishi kwa tabu huku kikundi cha watu kikitaka kuharibu amani ya nchi.
“Serikali ipo kazini na vijana (Polisi) wapo kazini, kinachotakiwa ni wananchi kutoa ushirikiano kuwasaidia askari wanaosaka wahalifu ili waweze kukamatwa,” alisema. Mwigulu alisema kinachoonekana wahusika wa mauaji ni wenyeji wa maeneo hayo kutokana na mauaji yanavyotokea kwani yanaonesha wenyeji wanashiriki na kama ni wageni wanakodiwa lakini wenyeji husaidia.
Alisema hilo lilijitokeza mgambo wawili walipouawa getini ambapo wauaji walienda kuwaita watu mitaani wakachukue mkaa. Alisema, watu walioitwa walikwenda kuchukua mkaa wakiacha maiti zimelala chini.
“Msako unaendelea na wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa askari na wasipoonesha ushirikiano, jeshi litatumia nguvu kuhakikisha wahalifu wanapatikana kwani wapo ndani ya jamii,” alisema.
Mwigulu alisema askari wanafanya doria Mkuranga, Rufiji na Kibiti kutafuta wahalifu ambao utafiti unaonesha wapo miongoni mwa wanajamii wanaoishi katika eneo hilo. Wabunge wahofia maisha yao Mbunge wa Rufiji Mohamed Mchengerwa ameiomba Serikali kuingilia kati na kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti mauaji yanayotokea katika wilaya tatu mkoani Pwani za Kibiti, Rufiji na Mkuranga kwa kuwa wananchi wa huko kwa sasa wanaishi kwa hofu.
Aidha, mbunge huyo amesema yeye pamoja na wabunge wenzake wa ambao ni mbunge wa Kibiti Ally Ungano (CCM) na mbunge wa Mkuranga Abadllah Ulega, wanaishi maisha magumu na ya taabu kwa sababu ya mauaji hayo.
Mchengerwa alikuwa akichangia bungeni Dodoma jana katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka wa fedha 2017/18. Alisema kwa sasa kila chombo cha habari kinaripoti matukio ya mauaji na mambo yanayoendelea katika wilaya hizo, hali inayoashiria wazi kuwa bado hali si shwari na hatua madhubuti zinahitajika.
“Watu wengi wamekuwa wakituuliza mbona hatuzungumzi leo nasimama hapa naiomba serikali itusaidie hali ni mbaya” alisema. Hata hivyo, alimshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kwa hatua aliyoichukua ya kutembelea waathirika wote wa mauaji hayo na kuwafariji jambo lililoleta faraja kwa wananchi hao. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, Taifa limeshuhudia mauaji ya kutisha ya askari polisi saba yaliyotokea wilaya ya Kibiti.
KWAHABARI,MATANGAZO,NANYIMBO TUPIGIE 0623372368






Chapisha Maoni