RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo saa chache baada ya kamati maalum iliyoundwa kuchunguza kilichomo katika kontena 277 zilizozuiwa bandarini yakiwa na makinikia kuwasilisha ripoti yake kwake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Profesa Muhongo jana alasiri, takriban saa nne baada ya kumtaka kujipima na kujitathmini kama anafaa kuendelea na wadhifa huo kutokana na madudu yaliyoibuliwa na kamati hiyo. Balozi Kijazi alieleza kuwa, nafasi ya Muhongo ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Vijijini, mkoani Mara, itajazwa baadaye.
“Profesa Muhongo nampenda sana na namheshimu sana na pia ni rafiki yangu, lakini kwa hili namwomba ajifikirie na ajitathmini kama anafaa kuendelea na wadhifa wake, binafsi namtaka aachie ngazi,” alisema Rais Ikulu jana mara baada ya kupokea taarifa hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Abdulkarim Mruma.
Baadaye jana ilipatikana taarifa ya barua kupitia mitandao ya jamii inayoaminika kutiwa saini na Waziri wa Nishati na Mdini, Pofesa Muhongo akiomba kujiuzulu wadhifa wake huo kwa Rais Magufuli.
Safari ya Uwaziri ya Muhongo Mei 2012, Rais Jakaya Kikwete alimteua Profesa Muhongo kuwa Mbunge, uteuzi alioufanya pia kwa Janet Mbene na James Mbatia. Baadaye alimteua kuwa Waziri wa Nishati na Madini. Hata hivyo, Januari 24, mwaka 2015, Muhongo alimuandikia barua Rais ya kujiuzulu kutokana na sakata la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani Oktoba mwaka 2015, alimteua tena Mhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini hadi jana alipotengua uteuzi wake kutokana na kutowajibika katika usimamizi wa rasilimali hiyo ya makinikia ya dhahabu. Licha ya Profesa Muhongo kutakiwa aachie ngazi, Rais pia ameivunja Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) iliyokuwa inaongozwa na Charles Sabuni.
Uteuzi wa Bodi Oktoba 12, mwaka jana Profesa Muhongo, alimteua Sabuni kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TMAA na uteuzi huo ulikuwa wa miaka mitatu ukianzia Oktoba 11, mwaka jana hadi Oktoba 10 mwaka 2019.
Mbali na Sabuni ambaye ni mwenyekiti, wajumbe wa bodi ni Dk Evelyn Richard, Dk Augustine Hangi, Dk Isaac Marobhe, Casmir Nkuba na Fatma Chillo. Mwingine aliyetumbuliwa na Rais Magufuli kwa uozo huo ni Mtendaji Mkuu wa TMAA, Dominic Rwekaza.
Mtendaji huyo amesimamishwa kazi, lakini Rais ameviagiza vyombo vya dola kuanzia jana kumchunguza yeye pamoja na watendaji na wafanyakazi wa TMAA ambao walikuwa wanashughulika na ukaguzi wa makanikia ndani ya migodi. “PCCB na vyombo vingine vya dola chunguzeni watumishi hawa kuanzia leo (jana) wahusika wote wafikishwe kwenye vyombo vya kisheria,” alisema Rais Magufuli.
Licha ya hatua hiyo, Rais pia ameviagiza vyombo vya ulinzi kuhakikisha kuwa vinahusika moja kwa moja katika masuala yote yanayohusu uchimbaji wa madini. “Tumejisahau sana, nawaomba muunde kikosi kazi ambacho kitashughulikia jambo hili ili raslimali zetu zisitoroshwe ovyo ovyo na kuishia nchi jirani,” alisisitiza Rais Magfuli “Ripoti hii haiwezi kupita hivi hivi, yaani tukiacha ipite hivihivi tutaonekana watu wa ajabu, we have to do something (lazima tufanye kitu) wakati tunasubiri ile ripoti ya kamati nyingine,” alisema Rai.
Rais pia alisema kwamba mapendekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo, Serikali inayakubali na itayafanyia kazi . Kilichomponza Profesa Muhongo Rais alisema Wizara ya Nishati na Madini imeshindwa kuisimamia TMAA katika kuhakikisha kunajengwa kinu cha kuchenjulia mchanga wa dhahabu hapa nchini. Alisema wizara pia imeshindwa kufuatilia utaratibu wa kusaifisha huo mchanga wa dhahabu ili kufahamu unakoenda.
“Kamishna wa madini anafanya nini? Waziri anafanya nini, naagiza tena vyombo vya ulinzi viwachunguze watendaji wote wanaohusika na sakata hili,” alisema. Alisema kilichomponyesha kamishna wa madini ni kutokana na kuteuliwa hivi karibuni hivyo hawezi kumhusisha kwenye sakata hilo.
“Ukienda hospitali wagonjwa wanahangaika hakuna dawa, madawati hadi tuchangishane, tunahangaika kukopa ndipo tupate fedha za kujenga reli ya kisasa, wakati fedha zipo hapa, ila Watanzania waliopewa dhamana ya kulinda raslimali zetu ndio wanaihujumu nchi.
Kwa kweli hili ni jambo la aibu, ndio maana siku ile nilimfukuza kazi yule katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini. Nilimwona anatoa majibu ya ovyo ovyo wakati anaulizwa na wabunge nikashindwa kuvumilia.
Haya mabilioni tunayopoteza hapa inaumiza sana… inaumiza sana, hawa wataalamu wetu ambao tumewapa dhamana ya kufanya kazi huko wamesahau hadi madini mengine hawayapimi wala kurekodi, hata haya ambayo TMAA wanarekodi wanakuja na kiasi kidogo.
“Tumeamua kuwaachia watu wachukue madini yetu, nchi yetu tulitakiwa tuwe donor country (nchi wafadhili) kutokana na mali hizi ambazo tumepewa na Mungu, lakini sisi tunagawa bure, sijui tuombewe kwa Imani gani.”
Alisema cha kusikitisha ni kwamba aliteua watu wasomi wazuri kusimamia rasilimali hiyo ya madini, lakini wame-prove failure (wameshindwa). Anasema viongozi wa wizara wameshindwa kusimamia TMAA hadi inashindwa kutekeleza majukumu yake.
Pia alisema Wizara ya Nishati na Madini imeshindwa kutekeleza ununuaji wa mtambo wa kuchenjua mchanga wa madini licha ya kuanishwa kwenye sheria ya madini ya mwaka 2009.
Alijihoji maswali kadhaa “Kwanini TMAA ipime sampuli kidogo na wakichukua sampuli wanaacha makontena bila kuyafunga. Kwanini wizara haikuwashitukia TMAA, kwanini bodi ya TMAA haikushituka, hapa unaweza kujihoji maswali mengi lakini hakuna majibu.”
Watanzania wamehongwa Rais Magufuli alisema jana wakati kamati maalum inaendelea na uchunguzi kuwa kuna Watanzania walitumiwa na wenye fedha kuwahonga ili kukwamisha kazi za kamati hiyo. Alisema kwa kutambua hilo, Serikali iliaamua kuwapatia ulinzi wajumbe hao ili wafanye kazi yao vizuri na kwa umakini bila kuingiliwa na mtu yeyote.
“Wapo waliotaka kuingilia uchunguzi huu na majina yao serikali inayo, wapo watu wamehongwa pesa na kuna wengine wamerekodiwa mpaka video! Ukiona mtu anabwatuka ovyo lazima ujue kuna kitu,” alisema Magufuli na kusisitiza kuwa wanayo majina ya Watanzania waliohongwa kukwamisha kazi za kamati hiyo.
Alisema nchi ipo kwenye vita mbaya ya uchumi, “ makontena 3600 ya mchanga yenye madini yanasafirishwa kila mwaka kwenda nje! Hebu pia hesabu kwa miaka 17 tumepata hasara kiasi gani?
KWA HABARI ZA BIASHARA ,MATANGAZO TUPIGIE 0623372368
Chapisha Maoni