VIONGOZI wa dini, wasomi na wanasiasa wamepongeza hatua hiyo ya Rais John Magufuli ya kuunda kamati na kuchukua hatua dhidi ya wizi unaofanyika kwenye makinikia maarufu kwa jina la mchanga wa dhahabu na kumtaka aichukue katika sekta nyingine kwani inaonesha jinsi nchi ilivyokuwa inaibiwa na kupoteza rasilimali zake.
Aidha, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto ameunga mkono matokeo yaliyobainishwa na kamati hiyo ya kuchunguza mchanga wa dhahabu na kubainisha wazi kuwa matokeo ya utafiti huo ndio rejea sahihi kwa sasa. “Utafiti unapingwa kwa utafiti.
Kwa sasa Kamati ya Mruma (Profesa Abdulkarim) ndio rejea sahihi kwenye suala la mchanga na hivyo nakubali mapendekezo yaliyomo,” alisema mbunge huyo wa upinzani aliyewahi kuwamo katika moja ya Tume za kuchunguza mikataba ya sekta ya madini nchini.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventisa Wasabato Jimbo la Kusini mwa Tanzania, Mike Malekana alisema hatua aliyochukua Rais dhidi ya watendaji wanaosimamia sekta hiyo muhimu ya madini, inastahili na ni ya kupongezwa.
Pia alisema wajumbe wa kamati waliofanya kazi hiyo wanastahili pongezi kwani wameifanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa. Alisema hatua ya Rais ya kuchukua hatua itafanya watendaji walio katika taasisi nyingine waogope na wafanye kazi kiadilifu.
“Naamini kuwa hatua hizi zitasaidia kuleta nidhamu serikalini hasa kwenye taasisi ambazo zinagusa rasilimali za nchi,” alieleza Malekana. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Dayosisi ya Mashariki na Pwani (KKKT), Dk Alex Malasusa alisema ripoti hiyo iwafumbue macho Watanzania hasa wanaofanya kazi kwenye sekta nyingine ambazo watu wana wasiwasi kuwa hazisimamiwi vizuri.
“Tuna maeneo mengi yanalalamikiwa, mfano kule baharini, vitalu vya uwindaji, Watanzania tunatakiwa kuwa wazalendo zaidi katika kulinda raslimali zetu,” alisema Dk Malasusa.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Uamsho la Moravian Tanzania, Emmaus Mwamakula alimpongeza Rais Magufuli kwa hatua hiyo aliyoichukua na hasa kuunda kamati ya kufanya uchunguzi na pia kupokea ushauri wa kamati hiyo.
“Huo ni utawala mzuri sana ambao Rais ameuonesha, kupokea ripoti ya kamati aliyounda, kupokea ushauri na pia kuchukua hatua,” alieleza Askofu Mwamakula. Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Method Kilaini naye amempongeza Rais kwa uamuzi wa kuwawajibisha viongozi ambao hawakutekeleza wajibu wao hata hivyo alishauri rungu hilo kuwafikia pia watu wote wanaosaini mikataba ya aina hiyo katika sekta ya madini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana mbali na kumpongeza Rais, alisema ripoti hiyo imewafumbua macho watu kwamba kuna mambo mengi yanaenda kiholela. “Alilofanya Rais ni jambo jipya, tumekuwa tukiwanyenyekea wawekezaji huku wakitunyonya,” alieleza Dk Bana.
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Humphrey Moshi alisema, “Nilitegemea mambo kama haya kwa sababu nimeandika taarifa nyingi kuonesha kwamba tunaibiwa kwenye madini, lakini hazikufanyiwa kazi.” Mwanasiasa Julius Mtatiro alisema ripoti hiyo imeonesha ni namna gani sekta ya madini imeibiwa na hiyo ni kutokana na mikataba mingi katika madini kutokuwa wazi.
Mwenyekiti wa Chemba cha Madini na Nishati Tanzania (TSME), Balozi Ami Mpungwe alisema hawajapokea ripoti hiyo, lakini watakapoipata na kuisoma watatoa maoni yao. Kwa upande wao, wabunge na baadhi ya mawaziri wamempongeza Rais Magufuli kwa hatua yake ya kuona kuna ukakasi katika suala la mchanga wa dhahabu na kuchukua hatua, hali iliyofichua madudu.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla alisema hatimaye Dk Magufuli amechukua hatua dhidi ya kelele zilizokuwa zikipigwa kwa muda mrefu na wabunge ambao awali walionekana mbumbumbu. “Ni ngumu kuamini kwamba wasomi wetu hawakuwa wanajua kwamba tunaibiwa. Wabunge tulisema tukaonekana mbumbumbu,” alisisitiza Dk Kigwangalla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dotto Biteko pamoja na kumpongeza Rais, alimshukuru kwa uamuzi wake kuchukua hatua za haraka dhidi ya wale wote waliohusika.
“Nampongeza Dk Magufuli kwa kuchukua hatua haraka kwa viongozi na wahusika wote wa madini na kwamba, hajamuonea mtu yeyote kwani hatua alizochukua ni kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati iliyobaini mambo mengi maovu ambayo viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini hawakuyaona wala kuyasimamia,” alisema Biteko.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe (CCM), alisema kutokana na matokeo yaliyobainishwa na Kamati iliyoundwa na Rais kuchunguza mchanga huo wa dhahabu, ni wazi kuwa nchi ilikuwa inaibiwa. Alisema mbaya zaidi hata kamati hiyo ilikuwa inapatiwa taarifa za uongo na wizara tofauti na hali halisi.
“Kilichokuwa kinatokea kwenye Kamati yetu ni kwamba wizara ilikuwa inaleta taarifa za uongo tofauti na hali halisi iliyopo katika wizara ila kamati iliyoundwa na rais imethibisha kila kitu, ni vyema viongozi tukabadilika kwani serikali hii sio ya mchezo,” alisisitiza.
Alisema endapo fedha zilizokuwa zinapotea zingepatikana, zingesaidia Watanzania na maisha yao yangebadilika. “Kwa hili Rais Magufuli wetu ameyaona ameamua kuwathibitishia Watanzania kuwa yeye ni kiongozi wa watu hataki mchezo na ameamua kuwajibisha watu palepale,” aliongeza.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel (CCM) alisema kutokana na yaliyobainishwa na ripoti ya Kamati hiyo, imewadhihirishia wazi kuwa Dk Magufuli ni Rais aliyechaguliwa na Mungu.
“Rais amethubutu; kwa hili anapaswa kupongezwa kwani kilichobainika leo kwa kweli pamoja na kusikitisha lakini kinadhidhirishwa kuwa tulikuwa tunaibiwa mbele ya macho yetu,” alisema Mollel.
Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) katika mtandao wake wa Tweeter pia amemuunga mkono kwa hatua alizochukua kuhusu suala hilo la mchanga. Katika mtandao huo, Nape pamoja na kuweka picha ya Rais Magufuli pia aliandika, “Kwa hili la mchanga…big up (hongera).”
Naye Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisema kilichobainishwa kwenye ripoti hiyo si jambo jipya kwani wabunge wengi walishakipigia kelele tangu awamu nyingine za serikali zilizopita.
Alimshauri Dk Magufuli kutowafumbia macho wale wote waliohusika na wizi huo wakiwemo mawaziri waliopita wa wizara hiyo wa muda mrefu kwa kufuatilia kikamilifu historia yake ili iwe fundisho.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kibamba John Mnyika (Chadema) ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia Wizara ya Nishati na Madini, alisema mzizi wa tatizo hilo ni Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na nyingine za kabla na mikataba mibovu.
Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Ngwali (CUF) alisema kinachotakiwa baada ya kubainika kwa wizi huo ni kuondoa mzizi wa tatizo na sio kuangalia kinachoonekana juu. Naye Mbunge wa Malindi, Ally Salehe (CUF) alibainishwa wazi kuwa amefurahishwa na hatua hiyo aliyoichukua Rais kwa kuwa sasa imebainisha wazi kuwa kuna wizi unafanyika katika mchanga huo.
Alisema japokuwa yamemkuta tayari Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, lakini walikuwepo mawaziri wengine wengi kabla yake ambao nao pia, wanapaswa kuchunguzwa na wakibainika kuhusika wachukuliwe hatua kali. Mbunge wa Pangani, Juma Aweso (CCM) alimpongeza Rais kwa namna alivyolishughulikia suala hilo kutokana na uzito wake.
Alisema hatua hiyo itawafungua macho Watanzania na sasa wataona namna rasilimali za nchi zinavyoibiwa. “Dk Magufuli ametunawisha sura, sisi kama wabunge tumeona mbele. Jambo lililomtokea Profesa Muhongo ni ajali ya kisiasa,” alisema Aweso.
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM) alisema kumekuwa na tetesi za muda mrefu kuwa kwenye mchanga kuna madini bila uthibitisho, lakini kupitia Kamati hiyo ya Rais leo (jana) Watanzania wamefumbuliwa macho.
Wakati huohuo, Mgodi wa Dhahabu wa Acacia ambao ni miongoni migodi iliyotajwa kuwa na mzigo katika kontena hizo, kupitia kwa Ofisa Habari wake, Necta Foya ulieleza kuwa upewe muda kuipitia taarifa hiyo kwani wameisikia, lakini wapewe muda waipitie zaidi. m Imeandikwa na Regina Kumba, Shadrack Sagati (Dar) na Halima Mlacha (Dodoma).
KWAHABARI ,BIASHARA NYIMBO TUPIGIE 0623372368






Chapisha Maoni