MTANDAO wa kutokomeza ndoa za utotoni Tanzania (TECMN) umeiomba Serikali kuweka mfumo madhubuti utakaowawezesha wanafunzi wa kike kuendelea kufurahia haki yao ya kupata elimu bora mara baada ya kujifungua.
Aidha, mtandao
huo umeshangazwa na kusikitishwa na kitendo cha baadhi ya wabunge kuunga mkono hoja ya kutowapa wanafunzi wa kike waliopata ujauzito wakiwa shuleni, nafasi ya kuendelea na masomo baada ya kujifungua kwake.
Mwenyekiti wa mtandao huo unaoundwa na mashirika 39, Valerie Msoka alisema hayo jana jijini Dares Salaam. Alisema tafiti zinaonesha asilimia 32 ya wasichana vijijini wameathirika na mimba za utotoni wakati waliopo mjini ni asilimia 19.
Alisema mkoa unaoongoza kwa mimba za utotoni ni Katavi kwa asilimia 45, Tabora asilimia 43, Dodoma na Morogoro asilimia 39, Mara asilimia 37 na Mbeya asilimia 32. Alisema kutokana na wasichana wengi kupata mimba na kukatiza masomo, wanaomba wabunge na wadau kupambana na changamoto zinazochangia ujauzito.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni ubovu wa miundombinu ya elimu, ukosefu wa elimu bora ya afya ya uzazi, umaskini, mmonyoko wa maadili, mila na desturi kandamizi na matumizi holela ya teknolojia.
Msoka alisema mtandao huo umeshangazwa na kusikitishwa na baadhi ya wabunge kuunga mkono hoja ya kutowapa wanafunzi waliopata ujauzito shuleni, nafasi ya kuendelea na masomo wakijifungua.
Walisema, hatua hiyo inarudisha nyuma jitihada za kuleta usawa wa kijinsia na kumuinua mwanamke kijamii, kisiasa na kiuchumi. “Haki ya kupata elimu bora ni haki ya msingi kwa mtoto hivyo kumnyima mtoto wa kike haki ya kuendelea na masomo kwa kigezo cha ujauzito ni ukiukwaji wa haki za mtoto na haki za binadamu,” alisema.
Alisema sababu zilizotolewa na wabunge ni za kisiasa zaidi zisizozingatia ustawi wa mtoto wa kike na mustakabali wa maisha yake na zinadhihirisha kutotambua viini vya matatizo yaliyoko katika jamii na kushindwa kushawishi njia bora zaidi za ya kuyatatua.
Alisema taasisi ya Utafiti ya kidemografia na Afya Tanzania inaonesha mwaka 2015/16 kuna ongezeko la mimba za utotoni katika maeneo mengi hasa vijijini. Msoka alisema utafiti huo unaonesha zaidi ya asilimia 27 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15- 19 wamepata ujauzito kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na ripoti ya mwaka 2010 inayoonesha asilimia 23.
Alisema kumnyima mtoto wa kike nafasi ya elimu kwa kigezo cha mimba ni kuendeleza umaskini, udhalilishaji wa kijinsia na kukwamisha jitihada mbalimbali za kimaendeleo, kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Chapisha Maoni