Image result for BUS LATAIFA STAR


KIKOSI cha wachezaji 20 wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars kinatarajiwa kuondoka leo jioni kuelekea Misri huku Nahodha msaidizi Jonas Mkude akikosa safari hiyo.
Taarifa ya Ofisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kwa vyombo vya habari jana, Alfred Lucas ilisema Mkude analazimika kubaki kutokana na ushauri wa Daktari aliyemtaka kupumzika kutokana na majeraha aliyoyapata katika ajali juzi.
Nahodha wa Simba, Mkude alikuwa miongoni mwa abiria sita waliopata ajali wakitokea Dodoma kwenye mechi ya fainali ya kombe la FA kati ya Simba na Mbao juzi ambapo shabiki mmoja wa Simba Shose ‘Wazza’ Fidelis alifariki dunia.
Simba ilishinda mabao 2-1. Stars inakwenda Misri kwa ajili ya kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Lesotho Juni 10, mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa, Dare s Salaam.
“Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga ameridhia Mkude kubaki na kusema kuwa ataungana na wenzake Juni 8 mwaka huu timu itakaporejea kutoka Misri. Mayanga hajajaza nafasi ya Mkude,” alisema.
Aidha, Mkude aliliambia gazeti hili jana muda mfupi baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu tangu juzi usiku kwamba ana majeraha kidogo shingoni lakini anaendelea vizuri.
“Nashukuru Mungu naendelea vizuri, daktari aliniambia sina tatizo kubwa ni mshtuko wa ajali na kwamba naweza kuendelea na ratiba zangu ndio maana nilikwenda kambini kuungana na wenzangu,” alisema.
Lucas alisema wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania Nahodha Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Faridi Mussa wataungana na wenzao moja kwa moja katika kambi ya Misri.
Katika mechi hizo za kufuzu, Tanzania imepangwa kundi L pamoja na Lesotho, Uganda na Cape Verde . Kikosi cha Taifa Stars kinaundwa na makipa Aishi Manula (Azam FC), Benno Kakolanya (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Haji Mwinyi (Yanga SC).
Walinzi wa kati Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Agrey Morris (Azam FC) ilihali viungo wa kuzuia ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude kutoka Simba SC ambaye hatasafiri na timu kwa sasa.
Viungo wa kushambulia ni Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC) na Mzamiru Yassin (Simba) wakati viungo wa pembeni ni Simon Msuva (Yanga SC), Shizza Kichuya (Simba SC) na Farid Mussa (Teneriffe, Hispania).
Washambuliaji wapo Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdurahman Mussa (Ruvu Shooting). Wasaidizi wa Mayanga katika benchi la ufundi ni Novatus Fulgence ambaye ni kocha msaidizi Patrick Mwangata - kocha wa makipa, meneja wa timu, Danny Msangi, mtunza vifaa Ally Ruvu, Daktari wa timu Richard Yomba na Daktari wa viungo Gilbert Kigadya.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top