Image result for SIMBA WAKIWA BUNGENI JANA
SIMBA, jana ilitinga bungeni na kushangiliwa na wabunge kwa kugonga meza kutokana na timu hiyo kutwaa ubingwa wa michuano ya kombe la FA kwa kuifunga Mbao mabao 2-1 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Wakiingia bungeni mjini Dodoma jana wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu, wabunge mashabiki wa timu hiyo, waligonga meza na kwa muda wa dakika moja, shughuli za bunge zilisimama kupisha shamrashamra za mashabiki hao.
Spika wa Bunge, Job Ndugai aliwauliza wabunge kwanini wanagonga meza, kuna nini kimetokea ndipo akabaini kwamba wachezaji wa timu ya Simba, viongozi na benchi la ufundi walikuwa wakingia bungeni ambapo aliwakaribisha akiahidi kuwatambulisha baadaye baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Wakati akitoa matangazo baada ya kipindi cha maswali na majibu kukamilika, Spika Ndugai aliitambulisha Simba kwamba ipo humo (Bungeni) ikiwa na wachezaji 23, viongozi na benchi na ufundi ambao ni wageni wa Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM).
Wachezaji wa timu hiyo, wakati wakisimama kuwasalimia wabunge ndipo wabunge waligonga meza kwa nguvu zaidi kwa dakika chache na Spika Ndugai akawapongeza kwa kunyakua Kombe hilo. “Nawatakia kila la heri Simba katika kushiriki katika michezo mbalimbali na hatimaye wachukue Kombe la Afrika,” alisema.
Kwa ubingwa huo Simba sasa itashiriki michuano ya kimataifa baada ya kukosekana kwa miaka minne. Aidha, Spika Ndugai aliipongeza pia Mbao kwa uchezaji wao na akawaomba waende wakajipande kwa ajili ya msimu ujao ili waendelee kufanya vizuri katika michezo mbalimbali nchini.
Lakini pia, Spika Ndugai alimpongeza Mbunge wa Nchemba, Juma Nkamia (CCM) kwa kukumbushia enzi zake za utangazaji kwa kutangaza mchezo huo mbashara kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Pia alisema, Timu ya Bunge Sports Club inaipongeza Simba Sports Club kwa kushinda mechi ya fainali dhidi ya Mbao FC 2-1 akaitaka Timu ya Mbao wasikate tamaa bali wajipande kwa mashindano ya mwakani.
Ndugai aliwapongeza wakazi wa Dodoma na vitongoji vyake kwa kujitokeza kwa wingi kuzishangilia Simba na Mbao katika Uwanja wa Jamhuri wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 17,000 ambao ulijaa pomoni.
Pia Spika Ndugai, alisema timu ya Bunge inampa pole mchezaji Jonas Mkude aliyepata ajali juzi wakati akirejea Dar es Salaam kwenda kujiunga na Timu ya Taifa, akataka apone haraka.
“Pia timu ya Bunge inasikitishwa na kifo cha mshabiki wa Simba, Shose aliyekufa katika ajali alimokuwa amepanda mchezaji Mkude na naomba roho ya marehemu iwekwe mahali pema peponi,” alisema Spika.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top