MIFUKO zaidi ya 19 yenye ukwasi wa Sh trilioni 1.3 imeanzishwa nchini kwa ajili ya kutoa ruzuku na mikopo kwa vikundi mbalimbali vya wajasirimali.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Antony Mavunde alitoa takwimu hizo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtambwe, Khalifa Mohamed Issa (CUF).
Issa alitaka kujua serikali itaweka lini mpango madhubuti wa kutoa elimu ya mikopo kwa wajasiriamali ili waweze kuandika michanganuo ya miradi ili wapate mikopo. Kuhusu mafunzo Mavunde alisema, katika Ofisi ya Waziri Mkuu kuna Baraza la Uwezeshaji Wananchi linalotoa mafunzo ya kiuchumi kusaidia wajasiriamali kupata taaluma ya kuanzisha miradi.
“Katika kila halmashauri nchini, kuna dawati la uwezeshaji linalofanya kazi ya kutoa elimu kwa wajasiriamali ili kupata elimu mbalimbali ikiwamo ya kuandika miradi,” alisema. Akijibu swali la msingi la Mbunge Issa aliyetaka kujua serikali itaweka mpango gani unaotekelezeka ili wajasiriamali waweze kukopa mikopo kutoka taasisi za fedha, Mavunde alisema, Serikali inawezesha wananchi ili kukopa kupitia sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2004 na sheria ya uwezeshaji wananchi namba 6 ya mwaka 2004.
“Sheria ya uwezeshaji wananchi imeainisha nia ya serikali ya kuweka kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa mitaji na kuondoa vikwazo ili benki ziweze kukopesha amana zilizopo kwa gharama nafuu kupitia vikundi vidogo, Saccos na vicoba,” alisema.
Alisema kutokana na sera hiyo, mipango, miradi na mifuko kadhaa imeanzishwa na serikali ili kuwezesha wananchi kukopa kwa urahisi, lakini pia inaendelea kusimamia mipango hiyo ili wananchi waendelee kunufaika na mikopo inayotolewa yenye masharti nafuu.
Mavunde alisema mfumo wa mabenki na taasisi za fedha kwa sasa unaendeshwa kwa utaratibu wa ushindani, hivyo viwango vya riba pamoja na masharti mengine huwekwa na taasisi husika ili kuhakikisha inapata marejesho.
Alisema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaendelea kuangalia viwango vya riba kwa benki na taasisi za fedha na katika kutekeleza hilo, imechukua hatua kupunguza riba kwa mikopo kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12,” alisema.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top