Vijana
nchini wametakiwa kutumia vyema mitandao ya kijamii kwa kujiongezea
ujuzi na kuwa wabobezi katika nyanja mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji
na teknolojia hatua itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Ushauri
huo umetolewa Jumamosi Oktoba 12, 2024 kwenye kongamano la maadhimisho
ya wiki ya vijana yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza kuanzia Oktoba
08-14, 2024 yakiwa na kaulimbiu isemayo “vijana na matumizi ya fursa za
kidigitali kwa maendeleo endelevu”.
Akiwasilisha
mada kwenye kongamano hilo, Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA), Mhandisi Imelda Banali alisema teknolojia pamoja na mitandao ya
kijamii ni fursa kwa vijana ikiwa wataitumia kwa weledi.
“Ndiyo
maana tumeanzisha klabu za kidigiti mashuleni ili kuwajengea uwezo
wanafunzi kutambua matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii lakini pia
tunawezesha vijana kufanikisha mawazo bunifu” alisema Mhandisi Banali.
Naye
Mkurugenzi wa kampuni ya ubunifu ya Sahara Venture, Jumanne Mtambalike
aliwaasa vijana kutumia vizuri rasilimali muda kwa kujifunza masuala
mbalimali mtandaoni badala ya kumaliza muda na bando kwenye mambo yasiyo
na tija.
“Hivi
sasa kila kitu kiko mtandaoni, mfano ukiingia Youtube unaweza kujifunza
masuala ya teknolojia, matumizi ya akili ‘Artificial Inteligence- AI
(Akili Mnemba) na ukapata ujuzi wa kubadilisha kabisa maisha yako.
Uamuzi ni wako, uingie Youtube kusikiliza muziki au fursa za mtandaoni
na kukuza ujuzi wako” alisema Mtambalike akiwahimiza vijana kuwa na
matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii.
Vijana
kutoka maeneo mbalimbali walishiriki kongamano hilo wakiwemo wanafunzi
kutoka shule ya sekondari Ibinza wilayani Ilemela ambao walikiri
kuhamasika na elimu waliyoipata kupitia kongamano hilo.
“Nimejifunza
kuchangamkia fursa mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii kama vile
kufuatilia matangazo muhimu ikiwemo nafasi za kazi. Lakini pia tunaweza
kupata elimu ya matumizi ya AI ambayo ni muhimu kwa wakati huu dunia iko
kidigitali” alisema Manyanda Alex.
Naye
Mwalimu wa shule hiyo, Magreth Kitondo alitoa shukurani kwa shirika la
KIVULINI kwa kuwezesha wanafunzi hao kushiriki kongamano hilo. Shirika
hilo limekuwa likiwajengea uwezo wanafunzi kutimiza ndoto na malengo yao
kitaaluma.
Maadhimisho
ya wiki ya vijana yalifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Tanzania,
Kassim Majaliwa Ijumaa Oktoba 11, 2024 katika uwanja wa Furahisha jijini
Mwanza ambapo alitoa rai kwa mashirika yanayotoa elimu kwa vijana
kuhakikisha hayakiuki maadili ya kitanzania.
Na George Binagi- GB Pazzo, Mwanza
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Imelda Banali akitoa mada kwenye kongamano la wiki ya vijana 2024/
Mwanafunzi Jackson Manyama kutoka shule ya sekondari Ibinza wilayani Ilemela akichangia hoja kwenye kongamano hilo.
Vijana wakifuatilia kongamano hilo lililofanyika ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza.
Waalimu na wanafunzi wakiwa kwenye kongamano hilo.
Wanafunzi kutoka shule ya sekondari Ibinza wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kushiriki kongamano la wiki ya vijana.
Wanafunzi kutoka shule ya sekondari Ibinza wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kushiriki kongamano la wiki ya vijana.
Chapisha Maoni