KUIMARIKA upatikanaji wa dawa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma nchini, kumeligusa shirika lisilo la kiserikali la Sikika na kubainisha kuwa limeridhishwa na hali ya sasa ya upatikanaji wa dawa nchini.
Aidha, limeishauri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kuimarisha usimamizi na matumizi ya dawa. Katika mazungumzo ya watendaji wa Sikika wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Irene Kiria na wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari nchini, kwenye ofisini za shirika hilo Kinondoni, Dar es Salaam jana, kwa mujibu wa ufuatiliaji wa Sikika, upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutoa huduma umeongezeka.
Sikika kwa mujibu wa takwimu zao ilisema upatikanaji huo umeongezeka kutoka asilimia 56 mwaka jana hadi kufikia asilimia 81 mwaka huu. “Hiki ni kitu kikubwa ambacho hakijawahi kutokea kwa miaka mingi, kwamba kuna dawa kwa wingi na wananchi wanazipata kwa bei ileile, na kwa urahisi, hili ni jambo kubwa kwake (mwananchi),” alieleza Kiria katika mazungumzo hayo.
Kutokana na hilo, Sikika limeipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa hatua ilizochukua kuhusu hali ya upatikanaji wa dawa, na pia kufurahishwa na uamuzi wa serikali wa kupanga bajeti ya dawa na kuitekeleza kikamilifu kinyume cha miaka ya nyuma. “Tulilalamikia hilo kwa muda na tunafurahi kusema kwamba fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya dawa kwa mwaka wa fedha 2016/17 zilitolewa kwa kiasi kikubwa kulinganisha na miaka ya nyuma.
Hii imeiongezea MSD uwezo wa kuagiza na kununua dawa, na hivyo kuongeza upatikanaji wa baadhi ya dawa vituoni,” alieleza Kiria katika mazungumzo hayo ambayo wahariri pia walichangia mjadala huo.
Katika mwaka wa fedha wa 2016/17 serikali ilitenga bajeti ya dawa ya Sh bilioni 251 kutoka Sh bilioni 89 za mwaka 2015/16. Katika mwaka huu wa fedha ulioanza Julai Mosi, serikali imetenga fedha nyingi zaidi kwenye ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ambapo Sh bilioni 236 zimetengwa kwa ajili hiyo.
Aidha, kwa mujibu wa Bohari ya Dawa (MSD), uanzishaji wa utaratibu wa kuagiza dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji viwandani umepunguza gharama za dawa kati ya asilimia 15 hadi 80, hivyo kuongeza upatikanaji wa dawa vituoni kwa gharama nafuu.
Sikika pia ilipongeza uamuzi wa serikali wa kupunguza ukiritimba wa MSD, kwa kuwa sehemu pekee ambapo vituo vilitakiwa kununua dawa, baada ya sasa vituo vya huduma kuruhusiwa kununua dawa kutoka kwa wauzaji binafsi pindi zinapokosekana MSD. Kwa upande wao, wahariri katika mazungumzo hayo walieleza kuwa ni muhimu dawa zinazopelekwa vituoni zikawa ni zile zenye uhitaji kwa maeneo husika na kuwapo na udhibiti wa bei za dawa.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top