TANZANIA imeanza majadiliano na Kamati Maalumu iliyoundwa na Rais John Magufuli na wawakilishi kutoka Barrick Gold Corporation juu ya biashara ya madini, yanayochimbwa na migodi ya kampuni hiyo nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana, mazungumzo hayo yalianza jana jijini Dar es Salaam na Kamati Maalumu ya Tanzania inaongozwa na Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi na Kamati ya kutoka Barrick Gold Corporation inaongozwa na Ofisa Mwendeshaji Mkuu, Richard Williams.
Taarifa hiyo ilimkariri Profesa Kabudi, akizungumza kabla ya kuanza kwa majadiliano hayo kuwa kamati yake imejipanga vizuri, kujadiliana na Barrick Gold Corporation juu ya madai ya Tanzania katika biashara ya madini ya kampuni hiyo nchini na itahakikisha inasimamia maslahi ya Tanzania ipasavyo. Kwa upande wake, Richard Williams alishukuru kuwepo kwa majadiliano hayo na amesema Kampuni ya Barrick Gold Corporation, imeyapokea madai ya Tanzania kwa mtazamo chanya na ipo tayari kujadiliana na kufikia makubaliano yenye maslahi kwa pande zote mbili.
Julai 10, mwaka huu akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Mazaina mjini Chato mkoani Geita, Rais Magufuli alizungumzia suala la serikali kuendelea kulinda rasilimali za Tanzania na kubainisha kuwa Julai 12, mwaka huu serikali ingekutana na wawekezaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, kuzungumza nao kuhusu kulipa fedha ambazo kampuni hiyo kupitia migodi yake nchini haikulipa wakati ikisafirisha makinikia (mchanga wa dhahabu) nje ya nchi.
Aidha, alisema tayari amesaini Miswada ya Sheria za Madini iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge mjini Dodoma, na sasa imeshakuwa sheria. “Nachukua fursa hii kulipongeza Bunge kwa kazi nzuri iliyofanya ya kupitisha Miswada ya Sheria mbalimbali za Madini na ninatamka wazi kuwa tayari siku ileile ya tarehe tano (Julai 5) nilipokabidhiwa sheria zile nilizisaini. Na keshokutwa (kesho) tutakuwa na mazungumzo na wale waliokuwa wanatuchukulia mali zetu,” alieleza Dk Magufuli.
Juni 14, mwaka huu, Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, ilisema ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake nchini.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Rais Magufuli kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Profesa John Thornton na kukubaliana kufanya mazungumzo na Tanzania, yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote, ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.
Rais Magufuli alisema serikali inakaribisha mazungumzo hayo; na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na Kampuni ya Barrick Gold Corporation, lakini pia alisema kuwa Profesa Thornton alikubali kushirikiana na Tanzania, kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu nchini.
Mei 25, mwaka huu, Rais Magufuli alipokea ripoti ya kwanza kutoka kwa Profesa Abdulkarim Mruma ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ambayo ilipewa kazi ya kuchunguza kiwango cha aina ya madini yaliyomo kwenye mchanga uliomo ndani ya makontena yaliyozuiliwa na serikali bandarini na sehemu mbalimbali nchini.
Kwenye ripoti yake ilibainika kuwa uwepo wa dhahabu kwenye makinikia ulikuwa ni mkubwa ambapo kwenye makontena 277 yaliyozuiliwa, kulikuwa na tani saba za dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1.147.
Aidha, Juni 12, Ripoti ya Kamati ya pili ya kuchunguza usafirishaji wa makinikia nje ya nchi ilikabidhiwa kwa Rais Magufuli, huku Mwenyekiti wake Profesa Nehemiah Osoro akisema Tanzania ilikuwa ikipoteza kati ya Sh trilioni 68.6 hadi Sh trilioni 108.5 tangu Acacia ilipoanza kuchimba na kusafirisha dhahabu nje ya nchi tangu mwaka 1998.
Mwekezaji huyo ambaye ndiye mmiliki wa migodi ya Pangea, Bulyanhulu na Buzwagi anadaiwa kuwa aliisababishia serikali hasara kwa kuipotezea mapato ya Sh trillion 68.59 ambayo ni makadirio ya chini wakati makadirio ya juu serikali ilipoteza Sh trilion 108.46. Wiki iliyopita, ilifahamika kuwa Barrick imepelekewa madai ya kodi ya Sh trilioni 424 na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na kushindwa kulipa kodi kwa kampuni zake tanzu.
Kampuni hizo ni Bulyanhulu Gold Mine inayoendesha mgodi wa Bulyanhulu na Pangea Minerals inayosimamia mgodi wa Buzwagi. Acacia ilionesha kushitushwa na deni hilo, lakini Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kwa msemaji wake, Benny Mwaipaja, ilikaririwa ikieleza kuwa deni hilo ni halali na lilikokotolewa kwa mujibu wa sheria na endapo kampuni hiyo ina tatizo, wanajua sehemu ya kwenda.
Chapisha Maoni