Magufuli aagiza kusimamishwa kazi kwa naibu kamishana wa uhamiaji
Image captionMagufuli aagiza kusimamishwa kazi kwa naibu kamishana wa uhamiaji
Rais John Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi kwa naibu kamishna wa uhamiaji kwa tuhuma za kuingiza nchini humo raia 50 wa Somalia na kuwapa vibali vya kuishi.
Kupitia waziri mkuu Kassim Majaliwa kiongozi huyo ametaka kusimamishwa kazi mara moja kwa bi Grace Hokororo na kuundwa kwa tume itakayochunguza utoaji wa vibali vya uraia nchini humo.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya kumaliza kikao na Makamishna wa uhamiaji kilichofanyika katika makao makuu ya uhamiaji jijini Dar es salaam.
Tayari Majaliwa amemuagiza waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba kubuni tume hiyo ya uchunguzi.
Amesema kuwa haiwezekani raia wa kigeni kuingizwa nchini humo na baadaye kupewa vibali vya kuishi bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kina."Idara ya Uhamiaji tunaitegemea kusimamia mipaka yetu na kuziba mianya ya watu kuingia bila ya kufuata taratibu lakini kwa mapenzi yake Ofisa huyu ameruhusu Wasomali kuingia bila kufuata taratibu."
Waziri Mkuu amesema ni lazima uchunguzi ufanyike ili kubaini ni kitu gani kilichomsukuma kuwapatia vibali Wasomali hao ambao hawakuwepo nchini.
''Wameingia na kupewa vibali moja kwa moja kwa mapenzi yake tu sasa hii ni dosari hatuwezi kuivumilia."
Amesema Serikali inaitegemea Idara ya Uhamiaji kwa kuzuia mianya ya uingiaji raia mbalimbali kutoka nje ya nchi bila ya kufuata taratibu.
"Hawa Wasomali aliowapa vibali vya kuishi wala hawakuwa wanaishi nchini wameingia tu na kupewa vibali, hivyo Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ameagiza ofisa huyo akae pembeni na achunguzwe ili kujua ni kitu gani kilimsukuma kutoa vibali kwa raia hao."
Pia majaliwa ameiagiza idara ya Uhamiaji kudhibiti kitengo cha utoaji hati za kusafiria za Kibalozi na kwa wanaomaliza muda kutopewa tena.
" Lazima hati hizo zikaguliwe katika mipaka yote na maeneo yote ya usafiri ili kujua kama huyo anayeitumia bado anahadhi hiyo na msiporidhika ichukuweni kwani kuna watu wanazitumia vibaya."
Hata hivyo Waziri Mkuu ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike kwa watu wote walioomba hati za kusafiria pamoja na vibali vya makazi iwapo wanakidhi matakwa ya kisheria kabla ya kuwakabidhi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top