MABADILIKO ya mfumo wa udahili kwa 
wanafunzi wa vyuo vikuu, yameibua matapeli wanaowarubuni waombaji wapya wa nafasi za masomo na kuwachukulia fedha badala ya kuwasaidia.
Kutokana na hali hiyo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimewataka wanafunzi wanaoomba kudahiliwa chuoni hapo kuwa makini na matapeli wanaowadanganya watoe fedha, kisha wakachukue fomu chuoni hapo.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Shahada za Awali chuoni hapo, Profesa Allen Mushi alipokuwa akizungumzia tatizo hilo baada ya kufikishiwa taarifa na baadhi ya waombaji wapya wa nafasi za masomo.
Alisema baadhi ya watu wanawadanganya wanafunzi wawape fedha, kisha waende kuchukua fomu chuoni hapo, jambo ambalo si la kweli, kwa kuwa mwaka huu udahili unafanyika kwa kupitia mtandao katika vyuo vyote.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja idadi ya waliokumbana na utapeli katika mchakato wa kuomba kudahiliwa chuoni hapo. “Katika kipindi hiki cha udahili kumetokea utapeli, watu wamekuwa wakiwahadaa wanafunzi kwa kuwapa utaratibu usio sahihi kisha kuwaibia fedha zao.
Mtu asikubali kutapeliwa kwani taratibu zote za wanaotaka kuomba watazipata kwenye mtandao wetu,” alisema. Alisisitiza kuwa mtandao huo, utakuwa wazi hadi Agosti 30 mwaka huu na baada ya hapo utafungwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kompyuta (UCC) chuoni hapo, Dk Elinami Minja alisema mfumo huo wa udahili kwa kuwa ni mpya, umekuwa na changamoto na kwamba tayari wameanza kuzishughulikia.
Alisema hadi kufikia kesho jioni (leo) mfumo huo utakuwa umetengemaa. “Kuna changamoto wakati wa udahili zilizojitokeza ambazo wanajitahidi kuboresha. Watu wawe na subira na kila mwombaji anapopata changamoto awasiliane na namba sahihi tulizozitoa.
Mfumo wetu wa mawasiliano sio wa haraka kama wengine, ila waombaji tunawaomba wawe wavumilivu,” alisema. Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa UCC, Elias Mturi alikiri wana changamoto kwenye hatua ya malipo, ambapo kuna ucheleweshaji unaomfanya mwombaji asiende kwenye hatua inayofuata.
Alikiri ucheleweshaji huo wanaufanyia kazi, na mpaka jana walikuwa wakitatua changamoto hiyo hali na kukiri ifikapo leo jioni itakuwa imekwisha. Mpaka jana asubuhi waombaji 15,900 walikuwa tayari wamejidahili kwenye mfumo huo chuoni hapo, na mwaka jana chuo kikuu kilisajili wanafunzi 9,200.
Zuio la kudahili Katika hatua nyingine, Kiongozi katika Mchepuo wa Madaktari Chuo Kikuu cha IMTU, Isaac Umapathy alisema kuwa hatua ya kufungiwa kudahili wanafunzi mwaka huu, imewaathiri katika utendaji wao, jambo ambalo wanaendelea kuwasiliana na mamlaka husika ili waruhusiwe kudahili wanafunzi.
Alisema, baada ya maonesho ya vyuo vikuu yanayoendelea viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, wanatarajia kukutana na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa ajili ya kujua hatma yao baada ya kukata rufaa.
Alisema kama hawataruhusiwa wataathirika vibaya kama chuo, lakini pia taifa litapoteza wataalamu wanaopatikana kila mwaka. Mkurugenzi Masoko wa Chuo Kikuu cha Kampala Tawi la Tanzania (KIUT), kinachosajili kati ya wanafunzi 2,500 na 3,000 kwa mwaka, Nuru Rashid alisema uamuzi wa Serikali wa kuwafungia wasidahili mwaka huu umewarudisha nyuma miaka 10, ila amewaomba wanafunzi wanaoendelea kusoma, wawe watulivu waendelee na masomo yao.
Alisisitiza watafuata maelekezo yote waliyopewa na mamlaka husika na imani yake ni kwamba baada ya siku chache, watajua hatima yao, kama wataruhusiwa kudahili ama la.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top