SASA ni wazi kuwa nahodha msaidizi wa Yanga, Haruna Niyonzima amefunguliwa njia kuelekea Simba baada ya uongozi wa klabu hiyo kutangaza rasmi kuachana naye. Kwa zaidi ya wiki ya pili sasa kumekuwa na taarifa za Niyonzima kuachana na mabingwa hao wa Ligi Kuu na kujiunga na mahasimu wao Simba.
Taarifa ya katibu mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa kwa vyombo vya habari jana, ilisema klabu hiyo imeshindwa kufikia dau alilotaka mchezaji huyo ili kusaini mkataba mpya wa miaka miwili baada ya ule wa awali kutarajiwa kumalizika mwezi ujao.
Habari kutoka Yanga zinasema Niyonzima anataka kulipwa dola za Marekani 60,000 (Karibu sh milioni 120) ili aongeze mkataba, lakini taarifa nyingine za uhakika kutoka Simba zinasema tayari walishamalizana na mchezaji huyo tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Niyonzima ambaye amekuwa mchezaji wetu kwa misimu sita mfululizo katika kiwango bora bado ana mkataba na Yanga mpaka Julai, lakini hatutaendelea kuwa naye msimu ujao kwani hatukuweza kufikia muafaka katika mazungumzo yetu licha ya kuwa na nia ya kuendelea naye misimu miwili ijayo, klabu inamtakia kila la heri katika maisha yake ya soka,” alisema Mkwasa kwenye taarifa hiyo.
Niyonzima aliyejiunga na Yanga misimu sita iliyopita kama kiungo mchezeshaji akitokea APR ya Rwanda ameisaidia klabu hiyo kushinda mataji sita ambapo kati ya hayo manne ya Ligi Kuu Tanzania Bara, moja la Kagame na moja la Kombe la Shirikisho Azam (FA).
Aidha, habari za muda mrefu zinasema Yanga imemsajili Ibrahim Ajibu wa Simba ambaye naye anadaiwa kutaka dau kubwa ili kubaki Simba. Uongozi wa Simba ulikaririwa uko tayari kumruhusu Ajib kwenda anakokutaka kwa sababu wamempa dau lao na inaonekana hakubaliani nalo.
“Ajibu ni mchezaji mzuri na bado benchi letu la ufundi linamuhitaji, mkataba wake umekwisha tumemuwekea dau letu mezani hataki, basi hatuwezi kumlazimisha anaweza kwenda anakotaka,” alisema makamu wa rais Geofrey Nyange ‘Kaburu’.
Habari kutoka Yanga zinasema Ajibu ameshasajiliwa kwa sh milioni 50, na kwamba kinachosubiriwa ni mkataba wake na Simba kumalizika mwishoni mwa mwezi huu ndipo imtangaze.
Aidha, Mkwasa alisema usajili wa timu yake utaendelea kufanyika kwa wachezaji waliowalenga. Alisema baadhi tayari wamepata saini zao na wengine wanaendelea na mazungumzo kukamilisha utaratibu. Pia, alisema Kamati ya usajili inaendelea vizuri na harakati za kuwapata wale wanaohitajika kwa ajili ya kuboresha kikosi chao.
Chapisha Maoni