ALHAMISI wiki hii Rais John Magufuli alizindua mfumo wa ukusanyaji kodi za Serikali kwa njia za kielektroniki, unaosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA). Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo, Rais aliagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuta kampuni zote za simu za mkononi, zisizotaka kujiandikisha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na aliagiza kampuni mbalimbali kujisajili kwenye mfumo huo wa ukusanyaji kodi za serikali kielektroniki.
Tunaipongeza Serikali ya Rais Magufuli kwa kuwa mfumo huo wa ukusanyaji kodi za Serikali, utaondoa na kumaliza malalamiko yaliyokuwepo awali kwa wakusanya kodi na walipa kodi, waliokuwa wakisema wanatozwa kodi kutokana na makadirio ya juu kuliko halisi halisi ya biashara na mapato yao.
Tunasema tunapongeza kwa kuwa ni wazi mfumo wa uso kwa uso, ulikuwa na mapungufu makubwa. Moja ya mapungufu hayo ni mwanya wa mlipa kodi kutoa taarifa za uongo, hivyo kufanyiwa makisio ya chini, jambo ambalo ni mwanya wa kuiba pato la Taifa.
Mapungufu mengine yalikuwa mwanya mkubwa wa mlipakodi na mkusanya kodi, kushirikiana kudanganya Serikali kupitia rushwa. Mapungufu mengine yalikuwa baadhi ya walipakodi wasiotoa rushwa, kutakiwa kulipa kiwango kikubwa kuliko uhalisia, hivyo wengi kulazimika na kushawishika kujificha.
Sisi tunakubaliana na kauli ya Rais Magufuli kuwa mwarobaini wa malalamiko hayo, ni mfumo huo wa ukusanyaji kodi kielektroniki, kwa kuwa unatumia mashine kukokotoa hesabu bila kupendelea, wala kukandamiza mtu.
Tunaupongeza mfumo huu wa ulipaji kodi, kwa kuwa utaondoa mzigo wa kodi uliokuwa umetoa mwanya kwa ukwepaji; na hivyo mzigo mkubwa kubaki kwa wafanyakazi wanaokatwa mishahara ili kulipia kodi zao moja kwa moja kabla hawaijapokea.
Jambo hili sio siri, limeikosesha Serikali mapato mengi, ambayo yangeweza kutumika kuboresha huduma za kijamii na kujiletea maendeleo katika taifa. Kadhalika, tunasema tunaunga mkono wazo la Rais Magufuli la kuwasajili wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga ili wajulikane kwa vitambulisho halali kama walipakodi halali na hivyo walipe kodi zao na kuchangia pato la taifa.
Hili likifanyika, litaondoa mwanya wa ukwepaji kodi, unaodaiwa kufanywa na wafanyabiashara wengi, wanaowatumia wamachinga kwa malipo ya mfumo wa kamisheni, kuuza bidhaa bila kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Tunaamini kuwa suala hili likifanyika kwa dhati, litawezesha huduma na uboreshaji wa miundiombinu katika maeneo ya kufanyia biashara zao ili yavutie wateja na kuwaondolea adha ya mara kwa mara ya kuondolewa katika maeneo yasiyoruhusiwa kibiashara.
Hili pia litaondoa kero kwa watumiaji wengine, wakiwamo watumiaji wa njia na barabara zinazofungwa kwa biashara ya wamachinga katika mitaa kadhaa ya miji mingi. Miundombinu hiyo ikiimarishwa na kuboreshwa, itaimarisha usalama wa kimwili na kibiashara kwa wafanyabaishara hao.
Ndiyo maana sisi tunasema wazo la wamachinga kusajiliwa na mfumo wa kulipa kodi za Serikali kielektroniki, litatuongezea pato la taifa na kuchochea kasi ya maendeleo na ubora wa huduma kwa jamii.
Chapisha Maoni