Alisema hayo mjini Dodoma juzi wakati akiahirisha kikao cha Bunge hilo baada ya kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Alisema kamwe hatovumilia tena mbunge asiyeonesha nidhamu ndani ya Bunge hilo, ambaye anaonesha wazi kiburi. “Na nyie askari wa Bunge, wewe Sajini nataka nikisema mumtoe nje, mumtoe, si mnambembeleza, kama kazi imewashinda semeni, tulete kikosi kingine,” alisema Ndugai.
Aliwataka wabunge kufuata Kanuni za Bunge ikiwa ni pamoja na kuheshimu maamuzi ya kiti. “Mbunge anatakiwa akae Spika au mwenyekiti akisimama, na kama anaona imeshindikana kuwasilisha hoja yake ni bora atoke nje aende kantini akanywe chai kuliko kubaki na kufanya utovu wa nidhamu, hili halitavumilika,” alisema.
Spika alisema hayo baada ya kuibuka kwa vurugu bungeni, zilizosababisha mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) kutolewa nje ya Bunge hilo na askari kwa nguvu pamoja na kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge hilo kwa muda wa wiki moja kwa kitendo chake chake cha kukaidi amri ya kiti cha Spika.
Katika mtafaruku huo, ulitokana na mbunge huyo kutaka kumpa utaratibu mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde aliyekituhumu Chadema kuwa kwa kimekuwa kikimshambulia Rais John Magufuli huku chama hicho chenyewe kinatetea wezi.
Kutokana na hoja hiyo ya Lusinde, Mnyika aliomba kuhusu utaratibu kwa Spika, na kumueleza Lusinde kuwa hoja ya upinzani si kupinga hatua hiyo ya kuchunguza makinikia, bali ni kuitaka serikali ising’ang’anie eneo hilo dogo la mchanga; na badala yake iweke nguvu kwenye wizi mkubwa wa madini ya dhahabu yenyewe unaofanyika migodini.
Hata hivyo, baada ya hoja yake ya kuhusu utaratibu kukataliwa na Spika Ndugai kwa kutofuata Kanuni za Bunge kama zinavyotaka, wakati akikaa kumpisha Lusinde aendelee kuchangia, mmoja wa wabunge aliwasha kipaza sauti na kudai kuwa Mnyika ni mwizi.
Kauli hiyo iliamsha tahamaki kwa Mnyika, ambaye aliwasha kipaza sauti wakati mwenzake anaongea, akitaka aliyemuita mwizi abainishwe na athibitishe, jambo ambalo Spika alimwambia haliwezekani, kwa kuwa kanuni hazimtambui mtu anayeropoka ukumbini, bali wale wanaozungumza rasmi.
Kutokana hali hiyo, hali ya Bunge hilo ilichafuka, Mnyika aligoma kuzima kipaza sauti licha ya kuonywa zaidi ya mara tatu na Spika. Ndipo alipoamuriwa atolewe nje, ambako nako aligoma, akiendelea kudai ameonewa hadi alipobebwa msobemsobe na maaskari hadi nje.
Sakata hilo pia liliwahusisha wabunge wa Kawe, Halima Mdee na wa Bunda, Esther Bulaya (wote wa Chadema) ambao kwa nyakati tofauti wanadaiwa kushiriki katika vurugu hizo, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wabunge wenzao wa upinzani kutoka nje.
Kwa mujibu wa Spika, Mdee na Bulaya watajadiliwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ambayo itatoa maamuzi dhidi yao mapema siku ya Jumatatu.
Chapisha Maoni