KOCHA wa Tusker FC ya Kenya, George Best Nsimbe amejigamba kuifunga Yanga katika mchezo wa ufunguzi wa Mashindano ya SportPesa yanayotarajiwa kuanza kesho kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Nsimbe alisema hana wasiwasi na Yanga kwani wachezaji wa Yanga anawafahamu.
“Udhaifu wa wachezaji wa Kitanzania naufahamu hivyo sipati shida namna ya kuifunga Yanga kwani nia yetu ni kutwaa ubingwa,” alisema Nsimbe ambaye amewahi kuifundisha Azam FC.
Tusker FC yenye makao yake katika mtaa wa Ruaraka jijini Nairobi inaundwa na wachezaji wenye miili iliyojengeka na warefu Tusker FC inayodhaminiwa na SportPesa imeshinda taji ya Ligi Kuu Kenya mara 11 katika mwaka 1972, 1977, 1978, 1994, 1996, 1999, 2000, 2007, 2011, 2012 na 2016.
Baada ya mchezo kati ya Yanga na Tusker FC utafuatiwa na mchezo wa Singida United na AFC Leopards Simba inatarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza Jumanne dhidi ya Nakuru All Stars ya Kenya na Gor Mahia ikichuana na Jang’ombe Boys ya Zanzibar.
Bingwa ataondoka na zawadi ya sh milioni 66 zinazotolewa na Kampuni ya SportsPesa inayoendesha bahati nasibu nchini Kenya na hapa na inaidhamini Everton katika Ligi Kuu England ambayo itacheza na bingwa wa SportPesa Juni 13.
Chapisha Maoni