.

Image result for esta bulaya bungeni
WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Esther Bulaya wa Bunda Mjini na Halima Mdee wa Jimbo la Kawe, wamepigwa marufuku kushiriki shughuli zozote za Bunge hadi Aprili 2018 baada ya kudaiwa kufanya fujo bungeni kwa kudharau mamalaka ya Bunge.

Licha ya kukosa uwakilishi wa wananchi katika majimbo yao, kwa adhabu ya kusimamishwa kuhudhuria vikao na shughuli za Bunge kuanzia jana huku Mkutano wa Saba wa Bunge la Bajeti ukiwa umebakiza takriban siku 25, hawatahudhuria mikutano mingine miwili wa Nane, itakayofanyika Novemba mwaka huu na ule wa Tisa utakaofanyika Februari mwakani.
Kadhalika, wabunge hao watakosa posho yao ya kila siku ya kikao ambayo ni takriban Sh 220,000 na hawatahudhuria vikao vyoyote vya Kamati zao za Kudumu za Bunge pamoja na safari. Wabunge hao wameadhibiwa kutokana na kuonesha utovu wa nidhamu bungeni baada ya Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) kutolewa kwa nguvu nje ya Bunge.
Katika sakata hilo wakati anatolewa Mnyika, Mdee alionekana kumkaba mmoja wa askari wa Bunge kwa kumvuta koti kwa nyuma huku Bulaya akihamasisha wabunge wengine wa upinzani kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge, kugomea adhabu hiyo, aliyopewa Mnyika.
Awali, wakati wa mjadala wa Wizara ya Nishati na Madini, hasa wakati Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alipokuwa akichangia, wabunge wengi hasa wa upinzani, walikuwa wakisimama kutaka kumpa taarifa mbunge huyo ambaye katika mchango wake alijielekeza kuichambua hotuba iliyotolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara hiyo, John Mnyika.
Katika hali hiyo, Mnyika aligoma kutii agizo la Spika Job Ndugai aliyemtaka kuketi hata baada ya kupewa onyo na hatimaye, Spika akaagiza atolewe nje kwa kutumia askari wa bungeni.
Mbunge huyo wa Kibamba alikuwa analazimisha taarifa yake ipokelewa kuhusu madai kwamba kuna mbunge alikuwa amemwita mwizi. Chanzo cha hali hiyo kilikuwani hatua ya wabunge wa upinzani kuiponda ripoti ya Kamati Maalumu iliyoundwa na Rais John Magufuli ya kuchunguza kontena 277 za makinikia zilizokuwa katika Bandari ya Dar es Salaam.
Spika wa Bunge, Job Ndugai aliiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ikutane Jumamosi iliyopita na kuwataka wabunge hao wafike mbele ya Kamati. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, George Mkuchika alisoma maazimio yaliyofikiwa na kuwaomba wabunge wajadili kuhusu adhabu ilizopendekeza.
Kwa mujibu wa Kamati ya Mkuchika, ambaye ni Mbunge wa Newala (CCM), mapendekezo yao yalikuwa ni kutaka wabunge hao wasimame siku zilizobaki katika Mkutano wa Saba wa Bunge la Bajeti unaoendelea, na Mkutano wa Nane isipokuwa wafike siku ya mwisho ya mkutano huo.
Baada ya kusoma taarifa yake kabla ya kusoma maazimio, Spika Ndugai alitoa fursa ya Bunge kujadili taarifa hiyo ya Kamati ya Mkuchika. Wakati wa majadiliano, Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF), wa Ubungo Saed Kubenea (Chadema) na wa Malindi, Ally Salehe (CUF) waliomba Bunge lipunguze adhabu hiyo ya awali ya kutohudhuria Mkutano wa Saba na wa Nane isipokuwa wahudhurie siku ya mwisho.
Mtolea alisema kwa kuwa huu ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ni vema wabunge hao wakasamehewa, badala ya kuadhibiwa, huku akitaka wapewe adhabu mbadala. Hata hivyo, wabunge wengi akiwamo Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), Khadija Hassan Aboud (CCM) wa Viti Maalumu, Mary Chatanda wa Korogwe Mjini, (CCM), Mwanne Mchemba wa Viti Maalumu, (CCM), Ally Keissy wa Nkasi Kaskazini (CCM) na Jacqueline Ngonyani Viti Maalumu (CCM), walitaka adhabu hiyo iongezwe.
Katika mchango wake, Chatanda alipendekeza adhabu hiyo iongezwe kwa sababu wabunge hao wameonesha utovu wa nidhamu kupita kiasi, na vitendo vyao havikubaliki. Ngonyani alisema, “Hao sio wasichana, bali ni wanawake. Juzijuzi waliomba msamaha, tarehe mbili mwezi wa tano, sisi wote tukawatetea, sasa tena leo wamerudi, inaonekana ni mazoea. Waondolewe kabisa.”
Kutokana na wabunge wengi kulalamika kwamba adhabu haitoshi, Mbunge wa Viti Maalumu, Juliana Shonza (CCM) aliomba kubadilisha azimio lililotolewa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge bungeni na kutaka adhabu iongezwe.
Shonza alisema Bulaya na Mdee ni wazoefu, kwani wamekuwapo bungeni vipindi viwili, hivyo walitegemewa kuwa wangekuwa mstari wa mbele katika kutii maelekezo na masharti na Kanuni za Bunge ikiwa pamoja na kumheshimu Spika.
“Mara zote kunapotokea fujo bungeni, Mdee na Bulaya hawakosekani, lakini pia wamewahi kuadhibiwa na Bunge kwa vitendo vya utovu wa nidhamu na kudharau mamlaka ya Spika, kisheria ni wakosaji wazoefu,” alisema.
Mbunge huyo alishauri Bunge litoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wabunge hawa na wabunge wengine wanaofikiri kuwa Bunge ni genge ambalo mtu yeyote anaweza kulichezea na kulikosea heshima kila mara na kwa kadiri anavyotaka.
Shonza alisema adhabu hiyo ni ndogo, hivyo aliomba iongezwe kutokana na wabunge hao kurudia makosa hayo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu Mei 2 walipotenda kosa lingine.
Akitumia Kanuni ya Bunge 57(1), Spika Ndugai aliwahoji wabunge kama wanakubali hoja ya mbunge huyo ya kubadili adhabu iliyopendekezwa na Kamati, na wengi waliafiki hoja hiyo pamoja na ile ya kuongeza adhabu kwa Mdee na Bulaya.
Wabunge waliotaka adhabu iongezwe walishinda na Bunge liliridhia adhabu iongezwe kutoka mikutano mwili hadi mikutano mitatu kuanzia wa sasa wa Saba, wa Nane na Tisa na wabunge hao sasa watarudi Mkutano wa 10 ambao ni wa Bunge la Bajeti mwakani, hivyo watakosa takribani siku 53.
Akihitimisha kikao cha jana, Spika Ndugai alithibitisha kukosa huko vikao, akisema wabunge hao wataingia bungeni kwenye Bunge la Bajeti, Aprili mwakani. Alisema moyo wake umeridhika na adhabu hiyo kutokana na wabunge hao kwamba wamekuwa wasumbufu na mara kwa mara wamekuwa wakirudia makosa.
Spika alisema kama wabunge hao wa Chadema wanataka kwenda mahakamani wanaweza kwenda, na yuko tayari kutetea uamuzi huo wa Bunge. Kuhusu hoja ya Ally Salehe kwamba Mnyika alitolewa kibabe bungeni, Spika Ndugai alisema alimkataza mara kadhaa na akamtaka kutoka mwenyewe, lakini alikaidi.
Aidha, aliongeza kuwa hata askari waliomtoa nje walimtoa kistaarabu kama vile sio askari, na kutokana na kitendo hicho, ameamua kubadilisha kikosi kizima cha askari na ataendelea kufanya hivyo, kila inapobidi.
Bunge limeridhia adhabu ya Bulaya iongezwe kutokana na kuwa hilo ni kosa la mara ya tatu kutiwa hatiani kwa kosa kama hilo la kudharau mamlaka ya Spika na kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Mkutano wa Tatu na Nne wa Bunge na mara ya pili alisamehewa na kupewa karipio.
Bunge limeridhia Mdee kuongezewa adhabu kutokana na kuwa kosa hilo ni mara ya tatu kutiwa hatiani kwa kosa kama hilo la kudharu Mamlaka ya Spika na kupewa adhabu na Bunge.
Alishawahi kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Mkutano wa Tatu na Nne wa Bunge na mara ya pili alisamehewa kutokana na kuomba radhi Bunge kwa masharti la kwamba hatarudia tena.

Wakati uamuzi huo unasomwa na kutolewa bungeni, wabunge hao ambao pia kwa mujibu wa Mkuchika, hawakupokea samansi zao wala kufika mbele ya kamati hiyo, hawakuwapo bungeni.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top