WIZARA ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki imebainisha faida za ziara za viongozi wa kimataifa takribani 10 nchini pamoja na wajumbe mbalimbali kutoka nchi za nje, ambao wamefanikisha kusainiwa kwa mikataba takribani 40 ya miradi ya maendeleo.
Pamoja na hayo, wizara hiyo imesema Umoja wa Mataifa umepongeza juhudi za Rais John Magufuli, kutekeleza vyema kanuni za utalawa bora ndani na nje ya nchi. Waziri wa Mambo ya Nje na Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Alisema ujio wa viongozi na wajumbe hao nchini, umeiwezesha Tanzania kuimarisha uhusiano wake na nchi za viongozi hao kiuchumi, kijamii na kiusalama. Aliwataja viongozi waliofanya ziara kuanzia mwaka jana na mwaka huu kuwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi aliyewasili nchini Julai mwaka jana, na kufanikisha nchi yake kuipatia Tanzania mkopo wa riba nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 500.
Alisema fedha hizo ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika miji 17 ya Kasulu, Ludewa, Manyoni, Mugumu, Chunya, Sikonge, Makonde, Handeni, Wanging'ombe, Kayanga, Songea, Zanzibar, Geita, Kilwa Masoko, Makambako na Njombe.
Aidha, alisema ujio wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China ulifanikisha nchi hizo kuimarisha na kukuza uhusiano wa kiuchumi, kibiashara, kiutamaduni na kijeshi pamoja na uhusiano uliopo katika masuala ya kimataifa kwa manufaa ya nchi hizo zote mbili.
Alisema kupitia ziara hiyo, Tanzania imesaini mkataba wa msaada wa fedha za China Yuan 2,000,000 sawa na Sh milioni 633 kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya wageni mashuhuri Chamwino mjini Dodoma.
"Lakini pia Wizara ilifanikisha kuratibu ziara ya wajumbe wa Wataalamu wa mfuko wa maendeleo wa Kuwait uliokuja nchini Desemba mwaka jana, kwa lengo la kufanya tathmini ya miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa mfuko pamoja na kupokea maombi ya miradi mipya iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania," alisema.
Alisema kutokana na ziara hiyo, nchi hiyo ya Kuwait iliidhinisha mkopo wa kiasi cha Sh bilioni 110 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa barabara ya Chaya-Nyahua mkoani Tabora yenye urefu wa kilometa yenye urefu wa kilometa 84.4.
Pia, nchi hiyo ilianzisha kampeni ya maabara kwa shule za sekondari na kisima kwa shule za msingi. Kwa upande wa ziara ya Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi, ambaye ni Kaimu Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu iliyofanyika Oktoba mwaka jana, aliidhinisha kuipatia mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni 20 kwa ajii ya ujenzi wa barabara ya Malagarasi hadi Uvinza mkoani Kigoma yenye urefu wa kilometa 51.
Alisema katika jitihada za kuimarisha biashara baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu, Tanzania imealikwa kushiriki kwenye maonesho ya kibiashara yatakayofanyika Dubai mwaka 2020. Aliwahimiza wafanyabiashara wa Tanzania, kutumia fursa hiyo kwa kushiriki kikamiifu katika maonesho.
Balozi Mahiga pia alifafanua ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya Afrika na kubainisha kuwa kupitia ziara hiyo, Serikali ya Iran ilikabidhi msaada wa vifaa kwa Chuo cha Ufundi Stadi Mkokoton Zanzibar wenye thamani ya Dola za Marekani 500,000.
Aidha, serikali hiyo ya Iran iliahidi kujenga vyuo vya ufundi stadi katika maeneo ya Unguja na Pemba pamoja na kutoa fursa za mafunzo kwa Watanzana katika sekta za nishati ya mafuta na gesi.
Akizungumzia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila, Dk Mahiga alifafanua kuwa kupitia ziara hiyo nchi hizo mbili zilisaini makubaliano kushirikiano katika sekta za mafuta na gesi ambayo yatawezesha kufanyika utafiti wa mafuta na gesi katika Ziwa Tanganyika.
"Oktoba mwaka jana pia Mfalme Mohamed VI wa Morocco alifanya ziara nchini akiambatana na wafanyabiashara takribani 1,000 na kupitia ziara hiyo mikataba 23 ilisainiwa ya ushirikiano katika sekta za kilimo, uvuvi, usafiri wa anga, nishati, utalii, viwanda, fedha na bima.
Alisema pia Mfalme huyo wa Morocco alitoa ahadi ya kujenga uwanja Mkubwa wa kisasa wa mpira wa miguu mjini Dodoma na tayari eneo ambalo uwanja huo utajengwa limeshapatikana na timu ya watalaamu kutoka Morocco imeshafika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa ujenzi wa uwanja huo.
Kwa upande wa ziara ya Rais wa Zambia, Edgar Lungu, waziri huyo alifafanua kuwa kupitia wizara hiyo wakuu wa nchi hizo mbili walikubaliana sheria iliyounda Mamlaka ya Tazara ipitiwe upya ili kuboresha utendaji wa mamlaka hiyo.
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliyefanya ziara yake nchini Februari Mwaka huu, naye kupitia ziara hiyo Tanzania na Uganda zilisaini hati za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kisiasa, sekta ya biashara na uwekezaji, uchukuzi, mafuta na nishati.
Ziara nyingine ni ziara ya Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemorasia la Jamhuri ya Ethiopia, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, Makamu wa Rais wa Cuba, Salvador Valdes. Wengine ni Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Jamhuri ya Finland na ziara ya Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Uswisi na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.
Balozi Mahiga, kupitia ziara hizo katika kipindi cha mwaka 2016/17 wizara hiyo iliratibu na kusimamia kusainiwa kwa mikataba 12 na hati ya za makubaliano 28 baina ya Tanzania na nchi nchi mbalimbali.
"Mikataba na makubaliano hayo ni kiashiria kikubwa katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi yetu na nchi nyingine, mashirika ya kikanda na kimataifa, kuongeza kasi ya kuvutia wawekezaji, kukuza biashara na kutangaza utalii," alifafanua.
Alitaja baadhi ya mikataba iliyosainiwa kuwa ni hati ya makubaliano baina ya Tanzania na india kuhusu udhibiti wa rasilimali za majini, makubaliano ya kuondoa hitaji la visa kwa raia wa India na Tanzania wenye pasi za kidiploasia au za huduma na mkataba wa ushirikiano katika sekta ya mafuta baina ya DRC na Tanzania.
Pamoja na hayo, Balozi Mahiga alisema wizara yake imeunda timu ya watalaamu inayojumuisha wanazuoni kwa ajili ya kufanyia tathmini sera ya taifa ya maombi ya nje ya mwaka 2001 ili iendane na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yanayotokea ndani na nje ya nchi.
Kuhusu pongezi kwa Dk Magufuli, alisema pongezi hizo zilitolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alipokuwa njiani kwenda New York, Marekani. Aalisema Guterres, alipongeza jitihada za Rais Dk Magufuli kutatua migogoro ya kisiasa katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kufafanua kuwa Tanzania ilishiriki kikamilifu kutatua migogoro ya kisiasa ambapo Rais Mstaafu Benjamini Mkapa na Dk Magufuli walikuwa mstari wa mbele kurejesha amani katika nchi hizo.
Pia Balozi Mahiga alisema serikali itaendelea kudumisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa, mashirika ya fedha na mataifa mengine yanayolenga kuboresha huduma za kijamii. Akizungumzia ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema biashara baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imeongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 4.4 mwaka 2011 hadi kufikia dola za Kimarekani milioni tano.
Alisema kwa upande wa Tanzania biashara katika nchi za jumuiya hiyo iliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 787.1 mwaka 2011 hadi kufikia dola za Marekani bilioni moja mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 53.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeomba bajeti ya Sh bilioni 150.8 na kati ya fedha hizo, Sh bilioni 142.8 kwa matumizi ya kawaida na Sh bilioni nane za maendeleo.
Chapisha Maoni