MVUTANO umeibuka ndani ya Bunge kuhusu hatua ya Rais John Magufuli ya kuchunguza na kuzuia Makanikia nchini, kutokana na wabunge kutofautiana kutokana na hatua hiyo.
Mjadala mkali uliibuka bungeni Dodoma jana baina ya wabunge wa kambi rasmi ya upinzani na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), hadi kufikia kutumia lugha zisizoruhusiwa ndani ya chombo hicho wakati wakijadili suala hilo.
Mjadala huo uliibuliwa na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) wakati akichangia mjadala wa kupitisha Makadirio ya Mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki ya mwaka wa fedha 2017/18.
Alisema hali ya uchumi wa kidiplomasia nchini ni mbaya kutokana na mgogoro ulioibuliwa na ripoti ya kuchunguza Makanikia nchini iliyotolewa hivi karibuni, jambo lililoifanya kampuni ya Acacia kulalamika.
Alitahadharisha kuwa sura ya mgogoro huo, itapunguza kasi ya wawekezaji nchini. Hata hivyo, hoja hiyo ilijibiwa na mbunge wa Viti Maalum, Ester Mahawe (CCM) ambaye alisema si kweli kuwa hatua ya Rais Magufuli kuchunguza mchanga huo, inakimbiza wawekezaji kwani inadhibiti wizi wa rasilimali za Tanzania.
Alisema Rais anapaswa kupongezwa kutokana na uthubutu aliouonyesha, hali ambayo endapo itaungwa mkono na Watanzania wote itasaidia kulinda rasilimali za nchi na kuufanya uchumi wa taifa hilo kutengemaa tofauti na ulivyo sasa.
“Tumekuwa tunaibiwa kwa muda mrefu, nashangaa leo kuna watu humu ndani wanambeza Rais, kwa suala hili hata kama kutakuwa na athari tukubaliane kuzibeba wote athari hizo kwa faida ya taifa letu,” alisema.
Aliwataka wabunge wa upinzani kuacha kigeugeu, kwani wao ndio walikuwa wa kwanza kuilaumu serikali kuwa haichukui hatua za kulinda rasilimali za nchi, lakini hata baada ya serikali kuchukua hatua hizo, bado wameendelea kuilaumu.
Mbunge wa Mufindi Mjini, Cosato Chumi (CCM), aliwataka wabunge wasiichangie hoja hiyo kwa kutafuta ‘kiki’ (sifa), kwani suala hilo la makenikia kwa sasa linahitaji wananchi kuungana na kuwa kitu kimoja kwa ajili ya taifa lao.
Alisema kwa sasa ndio wakati muafaka kwa wanasheria waandamizi, kujitokeza na kujipanga kuitetea nchi yao kutokana na hatua ya Rais kutetea maslahi ya Watanzania.
Kwa upande wake, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), ambaye aliombewa mwongozo kwa matumizi yake ya lugha isiyokubalika bungeni, alisema anapinga maamuzi ya kutaifisha makanikia baada ya kutolewa kwa ripoti ya tume ya Profesa Abdulkareem Mruma.
Baada ya mbunge huyo kutoa kauli hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alimtaka mbunge huyo kuacha kutumia lugha za kuudhi.
“Tangu ameanza kuchangia amekuwa akitumia lugha ambazo si za kibunge, zinazodhalilisha na zenye kejeli, naomba mwongozo wako mheshimiwa mwenyekiti,” alisema Jenista.
Kutokana na kauli zake, Mwenyekiti wa Bunge, Musa Azzan Zungu alimkatisha na kumtaka atumie lugha yenye staha, jambo ambalo mbunge huyo alikubali na kuendelea na hoja yake.
Mbunge wa Viti Maalum, Juliana Shonza (CCM), alisema Tanzania imekuwa ni ya kwanza kukuza diplomasia ya kiuchumi na kubainisha kuwa anashangazwa na baadhi ya wabunge wanaopinga hatua ya Dk Magufuli aliyoichukua dhidi ya makinikia yaliyokuwa yanaibiwa.
Alisema wengi wa wabunge wanaompinga Dk Magufuli, ndio waliokua mstari wa mbele miaka ya nyuma kuilaumu CCM kwa kuchagua marais wadhaifu. “Leo hii tuna rais mchapakazi mwenye maamuzi magumu, tunasimama hapa kumpinga,” alisema.
Shonza ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), alisema ni kawaida kwa wapinzani kupinga kila kitu, hata kama ni kizuri na kwa bahati mbaya wamekuwa wakionyesha kuwa kuunga mkono zaidi matendo ya wizi badala ya kuyapinga.
Alisema Dk Magufuli ndiye rais anayefaa kwa sasa kuliongoza taifa hili na hata uamuzi aliochukua unapaswa kupongezwa, hakuna Mtanzania anayefurahia kuibiwa, hivyo wote wanapaswa kumuunga mkono. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM) alimpongeza Dk Magufuli kwa hatua aliyoichukua na kusisitiza kuwa kwa hatua hiyo rais amefungua milango ya uwekezaji wenye maslahi kwa taifa.
“Tusiogope katika hili nina hakika wawekezaji watakuja mezani, kumbukeni kwa sasa kote duniani sekta ya uziduaji (Extractive Industry) imebadilika. Huu ni wakati wa kuchukua hatua na si kutupiana lawama,” alieleza, Akifunga mjadala wa suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa serikali (AG), George Masaju, alisema ni mapema mno kuanza kuitupia lawama serikali kuhusu hatua hiyo, kwani endapo kutatokea tatizo lolote lazima litafanyiwa kazi.
Alisema suala hilo ni nyeti na linagusa maslahi ya nchi, hivyo linapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote. “Hoja kwamba nchi itashtakiwa haina mashiko kwani utekelezaji wa maagizo ya Rais yalizingatia sheria na mikataba iliyopo ambayo imetoa mwanya wa kufanyiwa 'review' kila baada ya miaka mitano,” alieleza.
Aliwataka wabunge hao kuacha kuchangia kwa kuwaogopesha wananchi kwamba nchi iko katika hali mbaya, jambo ambalo si kweli kwani taratibu zote zilifuatwa na nchi iko tayari kushughulikia changamoto zozote zitakazojitokeza.
“Serikali imefanya vyema katika hili kwani hata wenzetu tumewaambia tulichokiona na sasa tunasubiri tuwaambie nini kifanyike kuweka mambo sawa,” alisema. Kuhusu hali ya uwekezaji, alisema si kweli kuwa mazingira ya uwekezaji yameharibiwa na hatua hiyo ya Rais, kwani kwa sasa hali ni nzuri na wawekezaji wameendelea kuja nchini kila kukicha.
Awali, katika hotuba ya maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mchungaji Peter Msigwa, aliishauri serikali ihakikishe kuwa kwenye balozi zote za Tanzania zilizopo kwenye nchi 35 duniani, zinakuwa na mpango mkakati wa kukuza diplomasia ya kiuchumi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top