Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti cha Ukiliguru, Mwanza, Dk Simon Jeremiah (kushoto) ambaye ni mtaalamu wa mazao ya mizizi akizungumza na Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia nchini (OFAB), Philbert Nyinondi kwenye shamba la mihogo mkoani Kagera hivi karibuni.
MKOA wa Kagera ni miongoni mwa maeneo hapa nchini lililokabiliwa na upungufu wa chakula baada ya migomba inayozalisha ndizi ambalo hutumika kwa chakula na biashara kukumbwa na ugonjwa wa mnyauko.
Kutokana na hali hiyo kumekuwepo na jitihada za makusudi za kuhakikisha hilo linaendelea kuwepo ikiwa ni pamoja na kupanda mazao mengine mbadala ambayo yatatumika kama chakula na pia kuyauza. Mazao hayo mbadala ambayo yamekuwa yakihamasishwa kulimwa katika mkoa huo ni mihogo, viazi vitamu, viazi lishe pamoja na migomba iliyosafishwa kwa kutumia njia ya tishu culture.
Hivi karibuni, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), kupitia mradi wake wa Jukwaa la Bioteknolojia nchini (OFAB), ilituma watafiti na wataalamu wa kilimo mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu kilimo cha kisayansi kinachoweza kulimwa baada ya zao lililokuwa linategemewa kuvamiwa na magonjwa. Watafiti hao walitoka Costech na wengine kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiliguru Mwanza na Maruku Kagera.
Wataalamu hao walielezea mazao mengine mbadala ambayo yanaweza kutumika badala ya ndizi ili kukabiliana na njaa katika mkoa huo. Nayo ni muhogo, viazi vitamu na viazi lishe. Wataalamu waliokwenda mkoani Kagera walitembelea wilaya tano za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba na Biharamulo ambapo huko waliweza kutoa elimu kwa maofisa ugani pamoja na wakulima ya namna ya kutumia mbegu bora zinazokinzana na wadudu ambazo zimefanyiwa utafiti wa kisayansi.
Mratibu wa OFAB, Philbert Nyinondi anasema katika mkoa huo wa Kagera wamekuwa wakishirikiana na serikali za mikoa pamoja na wilaya kufanya mafunzo kwa maofisa ugani pamoja na wakulima kuonesha jinsi gani wanasaidia wakulima .
Nyinondi anasema baada ya wakulima kupata mafunzo hayo, wanapewa mbegu bora ambazo zitapandwa kwenye mashamba darasa ambayo yatakuwa ni mfano kwa wakulima wengine ikiwa ni pamoja na kuchukua mbegu bora kutoka kwenye mashamba hayo ambazo wanapewa na watafiti. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kyerwa, Kashungu Runyogote anaeleza kuwa sasa ni wakati wa wataalamu kuweza kusaidia ili waondokane na tatizo la njaa.
“Ardhi ya Kyerwa inafaa kulima mazao karibu yote yanayolimwa ulimwenguni lakini sijajua ni kwa nini tunang’ang’ania kulima zao moja. Viazi mviringo, vitamu, muhogo, maharage, njegele vyote vinastawi. Tatizo letu ni kuwa tulishika kitu kimoja ndizi lakini kwa sasa imeonekana imeshindwa kutusaidia,” anasema mwenyekiti huyo. Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Shaban Lissu anawashukuru wataalamu hao kutoka Costech na wengine kwa kufika na kuendesha mafunzo kwa maofisa ugani juu ya mbinu mbalimbali.
Lissu anasema huu ni wakati muafaka kwa wilaya hiyo kwani hakuna sababu ya kuwa na njaa. “Kyerwa bila umaskini inawezekana hivyo tufanye kazi. Huu ni muda muafaka kwa kufanyika mafunzo hayo ili kupata mbinu zaidi za kuzalisha na kudhibiti ugonjwa wa mnyauko. Ugonjwa huu wa mnyauko bado upo,” anasema. Anasema pamoja na kuwepo kwa ugonjwa huo wamekuwa wakifanya juhudi za makusudi ili kuhakikisha wanaudhibiti.
“Nasisitiza kuhusu zao la muhogo hapa linastawi, wataalam wetu pamoja wakulima tumelichukulia linaweza kuwa la biashara. FAO muhogo ni zao la tano kwa kuwa na kiwango kikubwa cha wanga. Pia inakadiriwa watu milioni 800 wanategemea muhogo duniani, milioni 500 wapo Afrika,” anasema. Anataja nchi zinazoongoza kwa Nigeria, Brazil, Indonesia, Thailand na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kaimu Mkurugenzi wa wilaya ya Karagwe, Walter Kirita anasema mpango huo wa watafiti kuwapa mafunzo umewafikia kwa wakati muafaka ikizingatiwa mkoa huo na sehemu kubwa ya Tanzania ulipatwa na ukame. Mkulima kutoka wilayani Karagwe, Adam Salum anasema karibu asilimia 95 ya wakulima wana shauku ya kurudi kwenye kilimo walichozoea cha migomba, hivyo anashauri waingie kwenye kilimo cha kisasa waachane na cha kizamani.
Mtafiti kutoka Costech, Dk Nicholus Nyange anasema nia yao ni kuona wakulima wanabadilika kuwa kilimo sio kile cha kujikimu bali cha biashara ili watakapolima kiweze kuwabadilisha wao na familia zao. Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti cha Ukiliguru, Mwanza, Dk Simon Jeremiah ambaye ni mtaalamu wa mazao ya mizizi anasema uzalishaji wa zao muhogo hapa Tanzania upo chini ya kiwango cha kimataifa.
Uzalishaji huu uko kati ya tani tano hadi saba kwa hekta ukilinganisha na uzalishaji wa kimataifa wa tani 10 kwa hekta Kwa maelezo yake, uzalishaji huu unakuwa chini kutokana na wakulima kutofuata kanuni za kilimo bora cha muhogo. Pia wakulima kutumia aina za kienyeji zenye uzalishaji mdogo. Anasema utafiti umeonesha kuwa muhogo unaweza kutoa mazao kuanzia tani 20 hadi 50 kwa hekta kama kanuni za kilimo bora zikifuatwa na wakulima wakatumia mbegu bora za muhogo.
Anasema ili mkulima apate ustawi mzuri wa zao hilo, sifa mojawapo ni kwenye vipanda vya muhogo, kwa maana kuwa kipando kinatakiwa kiwe na urefu wa sentimeta 25 hadi 30 ili upate ustawi mzuri, pia urefu wake hutegemea na umbali kati ya jicho na jicho na idadi ya macho inashauriwa kipando kiwe na macho kati ya matano hadi saba. “Idadi ya macho ni ya muhimu sana kwani ndicho chanzo cha mizizi na majani.
Vilevile ukomavu wa pingili ni kitu muhimu kuzingatiwa kwani huchangia kwenye ubora na wingi wa mazao yatakayovunwa,” anasema. Anaeleza mbegu bora za kupandwa zitokane na chanzo cha uhakika zilizosafishwa ‘tissue culture’. Pia zichaguliwe wakati majani karibu yote yapo ili kuondoa uwezekano wa kupanda mbegu zenye ugonjwa. Mtafiti huyo anashauri pia mbegu hizo zitoke kwenye mashamba yanayokidhi vigezo vya mashamba ya mbegu.
Anashauri katika mashamba ya mbegu, mkulima ajitahidi kuzuia wadudu na magonjwa kama batobato, michirizi kahawia, baka bakteria na wadudu kama vidungata, tanabui wa kijani, inzi weupe na panzi kunuka. Pia anawataka wakulima kuangalia historia ya eneo husika kama lina magugu hatari na wadudu au magonjwa kwenye eneo hilo ili kubuni mbinu za kuyazuia au kuyaangamiza kabla ya upandaji wa mihogo.
“Epuka kupanda muhogo kwenye eneo lenye mwamba chini kwani hii husababisha mizizi kutonenepa na kuwa na mavuno hafifu. Matuta yanahitajika hasa kwenye maeneo yenye chepe chepe ya maji kuzuia maji kujitenga na kuozesha mizizi au eneo lenye mvua kidogo ili kutunza unyevu,” anasema. Anaongeza kuwa shamba la muhogo linatakiwa kupandwa mwanzoni mwa msimu wa mvua ili kupata mavuno mengi ambapo ni Oktoba hadi Machi na Aprili.
Vile vile anawashauri wakulima kuchagua aina ya mbegu inayokua haraka na yenye wanga wa kutosha, pia yenye uwezo wa kukaa ardhini kwa muda mrefu kabla ya kuvunwa, inayoweza kuvumilia magugu, wadudu na magonjwa kwa kiwango kikubwa.

Anashauri mbegu bora za kupanda zitoke kwenye chanzo cha uhakika kama tishu culture, zichaguliwe zikiwa na majani karibu yote ili kuondoa uwezekano wa kupanda mbegu zenye ugonjwa na zitoke kwenye mashamba yanayokidhi vigezo vya mashamba ya mbegu. Anasisitiza kuwa umbali wa mashamba ya mbegu uwe mita 100 kutoka mashamba ya wakulima ili zisipatwe na maambukizi.IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI IMECHAPISHWA,MAY 24,2017
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top