FISTULA ni hali au madhara yanayowakumba wajawazito kutokana na uchungu pingamizi, yaani uchungu wa kujifungua wa muda mrefu. Hili ni tatizo linalowakumba na kuwaathiri wajawazito wengi duniani kiasi kwamba, mwaka 2003, Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) lilianzisha kampeni ya kulitokomeza katika nchi 50 ikiwamo Tanzania.
Nchini Tanzania, takribani wanawake 3,000 wanasemekana kuathiriwa na fistula huku nusu yao wakiwa hawajafikiwa wala kupata huduma za kuwasaidia kurudi katika hali yao ya kawaida.
Ikumbukwe mwathirika wa fistula hana uwezo wa kuzuia au kudhibiti haja ndogo wala haja kubwa ambayo hupitia njia zote za kujisaidia. Idadi hiyo ni mbali na wasiojulikana kutokana na wengine kufichwa badala ya kusaidiwa ili wapate huduma zitakazowaondolea tatizo hilo.
Ni bahati mbaya kwamba, baadhi ya watu wanaamini fistula haitibiki kitaalamu, ni ugonjwa wa aibu na wanaojua unatibiwa, hawajui matibabu yake ni bure, hivyo wanasita kujitokeza kupata huduma hospitali au vituo vya afya.
Zipo sababu kadhaa zinazochangia wanawake wanaoathirika na tatizo hili wengi kuwa wa vijijini na wanaotoka katika familia maskini. Mojawapo ya sababu hizo, ni ukosefu wa elimu sahihi, ya kutosha na endelevu kuhusu tatizo hili ikifuatiwa na umaskini unaokwenda sanjari na umbali mrefu unaowafanya akina mama wengi ambao ni wajawazito, kushindwa kufika katika vituo vya afya ili kujifungua au kupata msaada wanapoanza kuona dalili za hatari.
Tunaipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa juhudi inazozifanya kuhakikisha huduma dhidi ya tatizo hilo, zinapatikana katika maeneo mengi zaidi nchini kwa waathirika.
Tunaamini fistula ni janga linalowaathiri kwa namna moja au nyingine, wanajamii wote tangu mwathirika binafsi, ngazi ya familia na jamii nzima kiuchumi, kijamii au kisaikolojia. Ndiyo maana tunasisitiza kuwa, iwe ni fedheha kwa kila Mtanzania kumnyanyapaa, kumpuuza na hata kumtelekeza mwathirika wa fistula na badala yake, kila mmoja aone ni jukumu lake la msingi kumsaidia kuondokana na tatizo hilo.
Elimu kuhusu chanzo, namna ya kuepuka na madhara itolewe kupitia njia mbalimbali yakiwamo matumizi ya mabango, matangazo katika sehemu mbalimbali za huduma za kijamiii kama shule, zahanati, vituo vya afya na hospitali, sokoni na ofisi mbalimbali za Serikali.
Na ili elimu hiyo isambae zaidi, hata viongozi mbalimbali wakiwamo wanasiasa inafaa waelimishwe na kuagizwa kulifanya suala la fistula moja ya ajenda za kila mkusanyiko wao. Kampeni zinazohusisha vyombo vya habari na wasanii ziimarishwe, wataalamu waongezwe na vituo vya kutolea huduma kuidhibiti viongezwe.

Jamii ielezwe wazi matibabu na huduma dhidi ya fistula hutolewa bure katika hospitali zote. Ndiyo maana tunasema, wakati tukiadhimisha siku ya fistula jana tatizo hilo sasa liwe ajenda ya Watanzania mahali popote ili kuwapunguzia mateso wanawake kulinda nguvu kazi ya taifa.
IMEANDIKWA NA MHARIRI IMECHAPISHWA ,24,2017
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top