UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umesisitiza kuwa, bado unapambana kuhakikisha wanapata haki yao ya kurudishiwa pointi tatu walizopokwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, TFF, baada ya rufaa waliyoiwasilisha FIFA hivi karibuni.
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ amesema wamekuwa na mawasiliano mazuri na uongozi unaopitia kesi yao huko CAS, na wamepewa kauli ya matumaini kuwa imefika na siku chache zijazo majibu yao watapatiwa.
“Tumepata faraja kwa sababu tunachoamini Simba ndiyo timu inayostahili kuwa mabingwa kwa kumaliza ligi ikiwa na pointi 71, lakini tunashangaa TFF, kwenda kuwapa Kombe Yanga wakati wao ni washindi wa pili kwa sababu wamemaliza na pointi 68,”alisema Kaburu.
Kiongozi huyo amesema katika suala hilo hawatakuwa na mzaha hata kidogo, kwani kinachofanyika dhidi yao ni uonevu hasa ukizingatia ni kweli mchezaji waliyemlalamikia alikuwa ana kadi tatu za njano.
Alisema pamoja na mahasimu wao Yanga, kukabidhiwa taji, lakini hawatakata tamaa hadi hapo watakapo pokea maamuzi ya FIFA, baada ya barua waliyowaandikia wakipinga Yanga kupewa taji hilo wakati wao ndiyo mabingwa.
Simba ilifungwa na Kagera Sugar mabao 2-1 na baada ya siku tatu klabu hiyo iliwasilisha malalamiko kwenye Bodi ya Ligi kupinga ushindi wa Kagera kwa sababu ilimchezesha mchezaji Mohamed Fakhi aliyedaiwa kuwa na kadi tatu za njano.
Kamati ya Saa 72, iliipa Simba pointi hizo baada ya kujiridhisha, lakini uamuzi huo ulipinduliwa siku chache baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyopo chini ya TFF, kuirudishia pointi zake Kagera kufuatia hiyo kupinga kupokwa alama hizo wakidai mchezaji wao hakuwa na kadi tatu.
KWAHABARI MATANGAZO NYIMBO ZA SILI TUPIGIE;062337268






Chapisha Maoni