SERIKALI imetangaza kuanza kuwabana baada ya miezi sita, wamiliki wa viwanja vikubwa vilivyopo maeneo ya miji na majiji ikiwa hawaviendelezi kwa kuanza kuwatoza kodi ya ardhi hata kama vitakuwa havijapimwa.
Tayari serikali hiyo imetangaza kuandaa miswada ya sheria ya uendelezaji miliki, Sheria ya Utwaaji Ardhi na Fidia na Sheria ya Mawakala wa Ardhi kudhibiti sekta ya udalali katika upangishaji wa majengo na uuzaji viwanja. Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri William Lukuvi alisema watakaoshindwa kulipa kodi ndani ya mezi sita, viwanja vitataifishwa.
Alisema bungeni Dodoma serikali imejipanga kuhakikisha kila ardhi iliyopo nchini inapimwa na kutumika kwa usawa na haki kama ilivyokusudiwa. Lukuvi alisema kwa muda mrefu kumekuwepo na kilio cha wananchi wanavyokandamizwa na madalali hivyo sheria hiyo sasa itaweka masharti ya mtu mwenye sifa ya kuwa dalali tofauti na sasa yeyote anakuwa dalali.
“Serikali inakuja na miswada mbalimbali ukiwemo wa mawakala. Huu utawabana zaidi hawa madalali na kupunguza tatizo la wananchi kulizwa. Alisema madalali wengine hujinufaisha kupitia wananchi kwa kupiga mnada mali zao kwa mgongo wa mahakama bila kuwapa nafasi kujitetea. Alisema kutokana na matendo hayo na mengine yasiyofuata taratibu na kanuni, wananchi wengi wamelizwa mali zao na madalali hao huku wakiwa na haki, jambo ambalo sasa serikali imeamua kulivalia njuga ili likome.
Alitangaza vita dhidi ya wanaoitumia sekta ya ardhi kutakatisha fedha zao na akibainisha kuwa serikali imejipanga vyema kuwabana na kuwaumbua. “Tumejipanga kisheria, nawatahadharisha wale wote wanaokimbilia kwenye sekta ya ardhi kutakatisha fedha wajiandae,” alisisitiza Lukuvi. Kuhusu kodi ya ardhi kwa wamiliki wa viwanja vikubwa kwenye miji na majiji, alisema kuanzia Julai mwaka huu, wote watakaokuwa na maeneo makubwa wataanza kutozwa kodi ya ardhi hata kama hayajapimwa.
“Wapo wananchi wanaomiliki ardhi kuliko wengine lakini hao hao wanataka kuendelea tu kumilikishwa ardhi. Jijini Dar es Salaam wapo watu wanahodhi ardhi ekari mia mbili mpaka ekari mia tano, kule Lindi yupo mtu anamiliki ardhi ekari elfu nne, Kigamboni ekari elfu tano,” alieleza. Alisema watu wote wenye maeneo ya ukubwa huo bila kujali viwanja vyao vimepimwa au la watatozwa kodi kwa kuwa kumiliki maeneo makubwa bila kulipa kodi ni sawa na wizi kwa serikali.
“Pamoja na kuwalipisha kodi, nawapa muda wa miezi sita wasipoyaendeleza, tutayataifisha,” alieleza. Alisema mwaka wa fedha wa 2016/17 baada ya uhakiki wa viwanja na mashamba nchini alibaini kuwepo kwa ukiukwaji wa masharti ya umiliki. Alisema baada ya uhakiki huo, milki za viwanja 227 na mashamba 17 zilibatilishwa kwa ukiukwaji wa masharti.
Alisema viwanja na mashamba hayo vipo Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Iringa, Kagera na Morogoro. Alisema bado uhakiki unaendelea maeneo mengine ikiwemo Muheza, Mlalo na Korogwe na baadhi ya maeneo hayo yapo katika hatua za mwisho za kubatilishiwa milki kutokana na kukiuka huko kwa masharti ya umiliki. Alisema kupitia uhakiki wa mashamba ya uwekezaji kwa kushirikiana na halmashauri, mashamba 121 yaliyohakikiwa yakiwa na ukubwa wa ekari 552,139, kati yake 21 yako Tanga, Morogoro, Pwani, Njombe na Kagera.
Alisema kati ya mashamba hayo 121, mashamba 68 ndio yaliyoendelezwa na 58 yalitelekezwa na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wahusika. Lukuvi alibainisha mbele ya Bunge hilo, kuwepo kwa harufu ya rushwa katika viwanja vilivyopimwa na kugawanywa na Mamlaka iliyofutwa na Rais John Magufuli, ya Ustawishaji Makao Makuu ya Dodoma (CDA).
Alisema kwa mujibu wa taarifa ambazo wizara hiyo inazo, viwanja 60,000 vilipwa na CDA na kati ya hivyo, viwanja 26,000 viligawanywa kwa wananchi lakini viwanja 34,000 havijulikani vilipo zaidi ya kuwepo kwa taarifa za kugawanywa kwa wafanyabiashara wakubwa wa maduka. “Sasa hili tumelibaini. Viwanja hivi 34,000 tunaambiwa vipo kwa maduka fulani hivi, tunavifuatilia na wahusika tutawachukulia hatua. Lakini tunawatoa wasiwasi wakazi wa Dodoma, wale wote waliopatia viwanja na CDA watahakikiwa na kupatiwa hatimiliki ya muda wa miaka 99,” alisema.
Pamoja na hayo, alisema wizara hiyo imebaini kuwepo kwa baadhi ya taasisi binafsi zinazojihusisha na uandaaji wa ramani na kuziuza bila idhini ya Wizara ya Ardhi jambo ambalo ni kosa kisheria. Baadhi ya ramani hizo hazitoi tafsiri sahihi ya mipaka hasa mipaka ya Tanzania na nchi jirani. “Natoa rai kwa wote wanaojihusisha na shughuli hizo waache mara moja vinginevyo wizara haitasita kuwachukua hatua za kisheria,”alisema. Nayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka serikali kuweka pembeni tofauti za kiitikadi za kisiasa kunyang’anya mashamba yasiyoendelezwa.
Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Wilfred Lwakatare alisema kwa mujibu wa orodha waliyonayo mengi ya mashamba hayo yanahodhiwa na wanasiasa. “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka serikali ilete bungeni taarifa ya ukaguzi wa mashamba haya makubwa nchini ili ijadiliwe kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na Kamati Teule ya Bunge ya mwaka 2015,” alisema.
Kuhusu kodi ya ardhi, aliitaka serikali isitoze wamiliki wa maeneo yaliyopo katika miji na majiji hata kama viwanja vyao havijapimwa kwa kuwa ni kinyume cha Sheria ya Ardhi Namba 4 na 5 ya Mwaka 1999 inayotaka kodi ilipwe katika maeneo yaliyopimwa na kumilikishwa kwa kipindi maalumu. Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa Sh bilioni 70.7, kati ya fedha hizo Sh bilioni 45 matumizi ya kawaida na Sh bilioni 25 za maendeleo 2017/18.
KWAMATANGAZO YA BIASHARA WASILIANA NASI 0623372368
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top