APRILI 28, Mwaka huu, mjini Dodoma Waziri Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angella Kairuki, alimkabidhi Rais John Magufuli ripoti ya uhakiki vyeti vya watumishi wa Serikali ili kuwabaini waliogushi vyeti.
Wizara hiyo ya Ofisi ya Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi zilibaini watumishi wengi waliokuwa na vyeti vya kughushi jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi na hata maadili ya kijamii.
Katika makabidhiano ya orodha ya watumishi wenye vyeti hivyo feki, Rais Magufuli alisema, “Kuanzia sasa, hao watumishi 9,932 waondoke wenyewe kazini pamoja na kunyimwa mishahara yao ya mwezi huu (Aprili)…
Atakayekaidi hadi Mei 15, mwaka huu, naziagiza mamlaka husika kuwachukulia hatua kwa kuwafikisha katika vyombo vya sheria.” Niseme mapema kuwa, kama tunataka kuwa na taifa lenye maendeleo kwanza, tunapaswa kuwa wataalamu na hatuwezi kuwa wataalamu, kama hatuna elimu inayofuata misingi na taratibu zilizoainishwa hasa, katika kupata ajira.
Kwa kawaida, dawa ni chungu lakini inaponya ndiyo maana baada ya Rais kuchukua hatua hiyo ya kijasiri kuhakikisha “anasafisha nyumba,” wengi walimpongeza ingawa, hawakukosekana wachache waliolaumu kwa sababu zao binafsi. Hao, wamelaumu wakisema, wamelitumikia taifa kwa muda mrefu hivyo, hatua hiyo haikupaswa kuchukuliwa dhidi yao.
Jambo kubwa wanalolisahau ni ukweli kuwa, japo ni kweli wametumikia taifa kwa muda mrefu, lakini hawakutumikia kiadilifu ndiyo maana walifanya udanganyifu katika kuwasilisha nyaraka zilizotakiwa. Hapa ndipo penye funzo kubwa kwa umma. Kwamba, siku zote ni vema kuepuka njia za mkato kufika unapokusudia na ndiyo maana wahenga walisema, “Kawia ufike.”
Ninapata ujasiri kusema hivyo kwa kuwa athari za watu kudanganya na kuajiriwa kwa taarifa na nyaraka za uongo (feki) zimejionesha dhahiri katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na wengine kupewa nafasi wasizo na uwezo nazo na wengine, uzalishaji na utoaji huduma kuwa duni.
Hili limelitia hasara taifa kiuchumi na kijamii Kwa msingi huo, ni wakati mwafaka sasa kila mmoja kujua kuwa, kama tuko nyuma kimaendeleo na hata kiuchumi, tabia ya kughushi na kufanya udanganyifu imechangia ka kiasi kikubwa hivyo, kila mmoja aikimbie na isijirudie tena kwa Mtanzania yeyote.
Kadhalika, wazazi wawe mstari wa mbele kuhakikisha watoto na vijana wao wanajengwa katika mfumo wa kufuata taratibu, badala ya kuiga mambo ya mkato. Hili la udanganyifu, likatawaliwe na kila mmoja toka mwanafunzi, wazazi na wale na mamlaka husika.
Kwangu mimi, licha ya kuwaondoa kazini, wote waliofanya udanganyifu na waliowezesha kufanikisha udanganyifu huo, wanapaswa kushitakiwa kwa jinai waliyoifanya maana mchuma janga, hula na wa kwao.
Kama tutafanya kosa la kutojifunza kutokana na makosa hayo yaliyofanyika ambayo madhara yake tunayaona sasa yakituathiri kijamii na kiuchumi, tutakuwa sawa na sikio la kufa lisilosikia dawa
KWAMATANGAZO HABARI NYIMBO ZA ASILI WASILIANA NASI'0623372368
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top