OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) itawatuma wataalamu wa kitengo cha ufuatiliaji miradi katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro. Wataalamu hao watachunguza kwa kina gharama halisi ya Sh bilioni 12.6 za ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami nzito yenye urefu wa kilometa 4.8 katika manispaa hiyo.
Naibu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo alisema hayo juzi alipofanya ziara ya ghafla katika manispaa ya Morogoro, kuangalia mradi wa ujenzi wa barabara tatu tofauti kwa kiwango cha lami nzito.
Ziara hiyo ililenga kujiridhisha na madai yaliyotolewa bungeni juzi kuwa halmashauri hiyo inajenga ujenzi wa barabara ya lami nzito kwa gharama kubwa ya Sh bilioni tatu kwa kilometa moja na kuzidi hata kiwango cha Tanroads.
Naibu Waziri huyo alisema atakapoipitia taarifa ya timu ya mkoa iliyoundwa kuchunguza, jambo hilo pamoja na kukamilika kwa uchunguzi wa jambo hilo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro, wizara yake pia itatuma timu ya wachunguzi ili kujiridhisha na ubora wake kulingana na thamani halisi ya fedha zinazotumika.
Aliongeza kuwa kiuhasilia watu ambao si wataalamu wa masuala ya ujenzi wa barabara, unapotaja kuwa kilometa moja ya lami nzito inajengwa kwa kiasi cha Sh bilioni tatu , si jambo la kawaida na linatia shaka.
Naibu Waziri alisema suala hilo linahitaji kuwa na maelezo ya kina zaidi, ambayo yatawaridhisha wananchi na viongozi wengine ambao si wataalamu wa sekta ya ujenzi wa barabara za kiwango cha lami.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa hiyo, John Mgalula na Mhandisi wa Ujenzi, Godwin Mpinzile kwa nyakati tofauti walisema mbele ya Naibu Waziri kuwa mradi huo umegawanyika kwa ujenzi wa barabara tatu tofauti za kiwango cha lami nzito.
Mgalula alisema kuwa gharama hizo ni za uwekaji wa lami peke yake na miundombinu ya mifereji ya maji na taa za barabarani, ambapo ujenzi wa barabara ya Tubuyu yenye urefu wa kilometa 2.6 itagharimu Sh bilioni 5.1 ikijumuishwa lami nzito, ujenzi wa mifereji mikubwa ya maji na taa za barabarani.
Nyingine ni ya NaneNane yenye urefu wa kilometa 1.6 ambazo gharama zake ni Sh bilioni 3.2 zikijumuisha ujenzi wa mifereji na taa za barabarani; na Maelewano yenye urefu wa kilometa 0.6 ambayo gharama zake ni Sh bilioni 1.7 ikijumuishwa na uwekaji wa taa barabarabani na kujenga mifereji imara.
Alisema kuwa barabara hizo zinajengwa na Kampuni ya Ukandarasi ya China ya Group Six International Ltd. Katika ziara hiyo ya ghafla, Naibu Waziri aliongozana na Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo na Meya wa Manispaa hiyo, Pascal Kihanga.
Chapisha Maoni