PAMOJA na changamoto mbalimbali zinazoikabili Hospitali ya Taifa Muhimbili, kumekuwa na jitihada nyingi zinazofanywa na madaktari bingwa hospitalini hapo kwa ajili ya kupunguza gharama za wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Jitihada hizo zimetokana na matumizi ya teknolojia ya hali ya juu, ambayo madaktari wamepata kupitia ushirikiano wa nchi zilizoendelea katika sekta ya afya. Hivi karibuni, madaktari hao walionesha namna ya kufanya upasuaji wa matundu madogo bila kufungua tumbo, huduma ambayo awali haikuwepo.
Huduma hiyo inahusu kutoa uvimbe kwa akina mama, kufanya upasuaji wa kizazi na kutoa kizazi. Wagonjwa wengi wanahitaji hiyo ambayo itamsaidia mgonjwa wa upasuaji kwa njia hiyo, kutopoteza damu nyingi na muda mwingi wa kukaa hospitalini hapo.
Huduma hiyo inapunguza gharama za uendeshaji kwa sababu mgonjwa anaweza kufanyiwa upasuaji asubuhi na jioni akaruhusiwa. Tayari wagonjwa 16 wamefanyiwa upasuaji wa mishipa ya moyo bila kufungua kifua na huduma ya kuvuna mishipa kwenye miguu na kupandikiza kwenye moyo.
Huduma hizo zimekuwa zikiwapeleka wagonjwa wengi nje ya nchi, wakubwa kwa watoto, na kuigharimu serikali mabilioni ya fedha. Hata hivyo, bado kuna changamoto kadhaa ambazo zinatakiwa kutatuliwa ili kufanikisha utoaji wa huduma bora hospitalini hapo.
Viongozi wa hospitali hiyo wanapaswa kuwa na mikakati thabiti, kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa. Madaktari wanabainisha kuwa vyumba vya hospitali hiyo kwa ajili ya upasuaji vipo vya kutosha, isipokuwa vifaa havitoshi.
Mwenyekiti Bodi ya wadhamini wa hospitali hiyo, Profesa Charles Majinge, Anasema ni jukumu la hospitali na bodi kununua ili kuviongeza. Anasema kuwa vifaa vya kuanzia upasuaji vipo, lakini vinahitajika vingi na kujenga vyumba vingi zaidi ili kurahisisha utoaji wa huduma hizo.
Huduma hizo ni maendeleo ya elimu ya upasuaji, ambayo kwa nchi za Ulaya zinaitumia kwa asilimia 90. Changamoto nyingine ni kuiwezesha hospitali hiyo, kufanya kazi kama taasisi ambayo ina ubingwa wa hali ya juu na hospitali ya rufaa, ili kusiwepo wagonjwa wa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Katika kuthibitisha hilo, Profesa Majinge anasema wanakazania hospitali hiyo iweze kuleta huduma ambazo zilikuwa zinawapeleka wagonjwa nje ya nchi ziweze kufanyika hapa. Tunapaswa kuunga mkono jitihada hizi za serikali, ambayo inawaruhusu madaktari kutoka nje ya nchi kuja nchini; na hata waliopo kwenda nje kwa ajili ya kubadilishana uzoefu kuhusu sekta hiyo muhimu.
Tunatambua kuwa maendeleo ya Taifa hayawezi kuja, endapo kutakuwa na watu wenye afya dhaifu, hivyo huduma hizo za afya zinasaidia kuokoa fedha nyingi na maisha ya watu, ambao awali walikata tamaa kwa kukosa fedha kwa ajili ya kutibiwa nje ya nchi.
Ni rai yangu kwa watanzania ambao wanapata taarifa kuhusu utoaji wa huduma hizo, wasisite kufika Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu kwa kuwa wapo madaktari bingwa wenye uwezo mkubwa.
Naamini kuwa wauguzi na madaktari waliopo, pamoja na changamoto hizo, wataendelea kuchapa kazi zao kwa weledi na ari kubwa ili kuwasaidia watanzania wenye magonjwa mbalimbali.
Aidha, ninaiomba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuendelea kufanya jitihada za kutatua changamoto zinazoendelea kujitokeza katika hospitali hiyo ya Muhimbili, ikiwemo kuwapatia kwa wakati fedha zote zinazotengwa katika bajeti ili kununua vifaa na kufanya maendeleo mengine yanayohitajika.
Kufanya hivyo, kutasaidia kuweka mazingira bora na kuamsha ari na uwajibikaji zaidi kwa madaktari, wauguzi na hata kwa wagonjwa, kwa kuwa hospitali hiyo ya Muhimbili ndio kimbilio la watu wengi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top