MAHAKAMA ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, juzi imemhukumu kifungo cha miaka 60 jela Charles Chacha (46), mkazi wa kijiji cha Kitaramanka wilaya ya Butiama mkoani Mara, baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili, likiwemo la kubaka mtoto wake wa kuzaa.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Richard Maganga wa mahakama hiyo, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo bila kuacha shaka yoyote.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi, Thophil Mazuge, kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Mei 8 mwaka jana, muda wa saa 10 jioni akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Kitaramanka wilaya ya Butiama.
Mazuge alidai kuwa mshitakiwa huyo siku ya tukio alikuwa nyumbani hapo na binti yake mwenye umri wa miaka 13, ambapo alimuingiza chumbani kwake huku akimtishia kumuua kwa kumchoma na kisu.
Alidai mshitakiwa huyo alitimiza azma yake hiyo kwa kumuingilia kimwili, baada ya kumviua nguo zake na wakati akiendelea kumfanyia unyama huo binti yake, mmoja wa watoto wake aliinga ghafla chumbani humo na kumkuta baba yake akiendelea na kitendo hicho cha aibu.
Alidai kuwa taarifa hiyo ilimfikia mama mzazi wa mtoto huyo na baadaye ikafikishwa kituo cha polisi Kiagata, ambapo polisi walifika katika eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa huyo.
Chapisha Maoni