RAIS John Magufuli ametoa wiki mbili kwa Mhandisi Mshauri pamoja na Mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa ujenzi wa mabwawa matatu ya maji safi wilayani Handeni mkoani Tanga, kurudi mara moja katika eneo la ujenzi ili kukamilisha kazi hiyo.
Pia amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba kuwakamata wahusika hao ambao ni Kampuni za DON Consultant na TANSINO endapo watashindwa kutekeleza agizo hilo. Ametoa maagizo hayo jana wakati wa siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tano mkoani Tanga katika mkutano wa hadhara, uliofanyika Kata ya Vibaoni mjini Handeni.
Dk Magufuli alisema haiwezekani wananchi wa Handeni, kuendelea kusubiri maji kwa zaidi ya miaka mitano sasa wakati tayari serikali imeshawalipa jumla ya Sh bilioni 2.8 kwa makandarasi hao, ambao alisema wamefanya kazi ya ovyo. “Fedha ya serikali haipotei, huyu consultant (mshauri) na contractor (mkandarasi) nawataka ndani ya wiki mbili wawe wamerudi site (eneo la ujenzi), nataka waanze kuyachimba haya mabwawa kwa fedha zao wenyewe na baada ya kukamilisha na kupata certificate (cheti) ndipo tutawalipa shilingi bilioni moja na milioni mia mbili zilizosalia,” alisema Rais Magufuli.
Aliongeza, “Najua ukubwa wa tatizo la maji hapa, hivyo wananchi wa Handeni hawawezi kuendelea kusubiri maji kwa miaka mitano wakati fedha ya serikali imeliwa na watu wachache, jambo hilo halikubaliki, Tanzania siyo nchi ya kuliwa hela. Mimi mtumbua majipu nipo na wasipoenda kukamilisha ujenzi huu haraka, basi yatawakuta yaliyowakuta wakandarasi wazembe... endapo watakaidi agizo hili basi RPC Tanga nakuagiza uende kuwakamata ili waende gerezani kwa sababu sheria ni msumeno.”
Mradi huo wa ujenzi wa mabwawa matatu ya maji katika miji ya Mkata, Manga na Kwandugwa wilayani Handeni, ulipangwa kugharimu jumla ya Sh bilioni 4.1. Hadi sasa tayari makandarasi wameshalipwa Sh bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya kukusanya maji ya mvua pamoja na miundombinu ya kusambazia, lakini haukukamilika kwa wakati na hivyo kusababisha wananchi kuendelea kuteseka. Akiwa njiani kutoka Korogwe ambako alizindua ujenzi wa stendi mpya ya mabasi, Rais Magufuli alitoa msaada wa Sh milioni tano taslimu kwa Shule ya Msingi Misima kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya shule hiyo.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top