MATAYARISHO kwa ajili ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga yamekamilika kwa zaidi ya asilimi 95.
Ofisa mwandamizi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC), anayesimamia ujenzi wa bomba hilo, Goodluck Shirima aliiambia HabariLeo jana kwamba karibu kila idara iko tayari kwa hatua hiyo muhimu itakayofanyika Jummosi Agosti 5.
Jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo litawekwa na Rais John Magufuli kwa kushirikiana na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni katika kijiji cha Chongoleani ambako ndiko kunajengwa matenki ya kuhifadhia mafuta ghafi kutoka Uganda kabla ya kusafirishwa kwa meli kwenda ughaibuni.
"Baada ya hatua zilizopita, ile ya kukubali bomba lijengwe Tanzania na kisha marais wa nchi hizi kuingia makubaliano rasmi ya ujenzi wa bomba hili Mei 21 mwaka huu, hatua hii ya jiwe la msingi ndio inaonesha kuanza rasmi kwa ujenzi na hasa ukizingatia mvutano uliokiwepo awali wa bomba lipite wapi kati ya Kenya na Tanzani ," alisema Shirima ambaye pia ni mwanasheria wa TPDC.
Alisema hatua hiyo ya Jumamosi pia itafungua milango ya kutangaza kandarasi za ujenzi wa bomba hilo linalotakiwa kujengwa kwa haraka (fast truck) huku hatua zungine zinahusu mikataba mbalimbali kama ule wa nchi husika na makampuni yatakayoendesha mradi huo mkubwa utakaogharimu dola za Marekani bilioni 3.5 ikiendelea.
Mradi wa bomba hilo linalopita katika mikoa 8 ya Tanzania unatazamiwa kukamilika mwaka 2020. Mikoa hiyo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabor, Singida, Dodoma, Morogoro na Tanga.
Hatua hii ya kuweke jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta imekuja huku mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) wakiandaa Jukwaa la Biashara litakalorindima Agosti 17 hapa Tanga.
Jukwaa hilo litakaloshirikisha wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za fedha litasaidia kuibua fursa mbalimbali za uwekezaji na namna ya kupata fedha kwa ajili ya kuendeshea miradi. TSN inayochapisha magazeti ya HabariLeo, Daily News na SportLeo imeshaandaa majukwaa k ama hayo katika mikoa ya Simiyu na Mwanza na kutoa mafanikio makubwa kwa wananchi wa mikoa husika.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top