WIKI hii kulikuwa na sakata la aina yake, ambapo Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), imeanza kuvifungia baadhi ya vituo vya mafuta nchini, kutokana na kuuza bidhaa hiyo bila kuwa na mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFDs) za mamlaka hiyo.
Kampeni hiyo ilianza Alhamisi jijini Dar es Salaam, ambako vituo 13 vilitiwa kufuri na kuendelea juzi katika miji ya Tanga na Dodoma, ambako jumla ya vituo 33 vilifungwa. Katika Manispaa ya Dodoma, vituo 15 vilifungwa ambavyo ni vya kampuni za TIOT, Ibra General Enterprises, TSN, Oil Com (vituo 3), Camel Oil (vituo 2), Lake Oil (vituo 2), State Oil, GP 88 (vituo 2) na Afroil.
Kwa upande wa Tanga, vilifungwa vituo vya mafuta 18 ambavyo ni pamoja na TOC kilichopo Mtaa wa Donge, Ngamiani kilichopo Barabara ya 11, Tapco kilichopo Mabada ya Papa, Star kilichopo Barabara ya Saba, Lake Oil kilichopo eneo la Reli na Afro Oil.
Tunapongeza hatua hiyo kali iliyoanza kuchukuliwa na TRA, kwa sababu TRA inaifanya ili kutekeleza matakwa ya sheria. Kwamba wenye vituo vya mafuta nchini, walipewa muda wa kutosha kufunga mashine hizo, lakini hawajafunga hadi sasa.
Jambo lingine ni kuwa kabla ya kuchukua hatua hiyo, TRA ilifanya ukaguzi kwenye vituo mbalimbali vya mafuta ili kujiridhisha kama vinatumia mashine hizo. Pia, tunaunga mkono kauli iliyotolewa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo kwamba TRA haitatoa muda wa majadiliano ya ziada na wenye vituo vya kuuza mafuta, ambao wamekaidi kufunga mashine za kielektroniki kwenye pampu za kuuzia mafuta.
Kayombo anasema kwamba TRA imechelewa mno kufanya uamuzi wa kuwafungia watu hao. Anasema TRA imekuwa na huruma kupita kiasi, kwa sababu watu hao walitakiwa wawe wamefunga mashine hizo tangu Septemba mwaka jana, lakini hawakufanya hivyo.
Ikumbukwe pia kwamba mwaka jana mwanzoni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango aliwapa wamiliki hao muda wa nyongeza kuanzia Julai 16 hadi Septemba 16, 2016 wawe wamefunga mashine hizo kwenye pampu za mafuta.
Hata hivyo, wengi wao hawakutekeleza agizo hilo la waziri, isipokuwa wachache tu ambao ni pamoja na Puma, Total na Gapco, waliotii na kufunga mashine hizo mapema. Aidha, sheria ya kutumia mashine za EFDs kwenye vituo vya mafuta nchini, ilitakiwa ianze kutekelezwa tangu mwaka 2014.
Lakini, TRA iliona ni busara kujadiliana kwanza na wamiliki wa vituo vya mafuta. Kuna baadhi watu, mfano Chama cha Wamiliki Wauza Mafuta Rejareja (TASDOA), wamekuwa wakidai kuwa mashine hizo za EFDs ni ghali na kwamba wapo kwenye mazungumzo na TRA.
Lakini, Kayombo anasema madai hayo ni ya uongo na visingizio tu visivyo na sababu za msingi. Kwa mujibu wa Kayombo, hivi sasa mashine moja ya EFD, inafungwa kwenye pampu nne za mafuta.
Hivyo, kama kituo kina pampu nane, mashine zinazohitajika kwenye kituo kizima ni mbili tu. Kwamba wauzaji hao wanatafuta visingizio visivyo na sababu za msingi. Tunataka wamiliki wa vituo vya mafuta kutii sheria, kwa kufunga haraka mashine hizo. Aidha, tunahimiza uhakiki wa mashine hizo, uendelee nchi nzima na uwe endelevu.
Chapisha Maoni