Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amelitaka Jeshi la Polisi kumuondoa katika nafasi ya Mkuu wa Polisi, Usalama Barabarani (RTO) Mkoa wa Pwani kutokana kwa kushindwa kusimamia sheria za usalama barabarani mkoani humo.
Masauni alitoa agizo hilo katika Kituo cha Mabasi cha mjini Kibaha Maili Moja baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kituoni hapo jana, kwa ajili ya kufuatilia maelekezo yake aliyoyatoa alipofanya ziara kama hiyo mwaka jana.
“RTO ameshindwa kuendana na kasi ya awamu ya tano, nataka aondolewe katika nafasi hiyo na achukuliwe hatua ya kinidhamu, hatutaki uzembe, hatutaki kucheza na maisha ya watanzania,” alisema Masauni.
“Mwaka jana nilipofanya ziara kituoni hapa nilitoa maelekezo nilipokuta kuna mapungufu katika ukaguzi wa magari, tukakubaliana atayafanyia kazi haraka iwezekanavyo, lakini hakuna mabadiliko yoyote, magari hayakaguliwi, huku ni kuhatarisha usalama wa abiria.”
Aidha Masauni mara baada ya ukaguzi wa kituo hicho, aliendelea na ziara yake mkoani Pwani ambapo alifanya ukaguzi wa aina hiyo mjini Chalinze na baadaye Msata na kuimalizia ziara yake Bagamoyo.
Chapisha Maoni