West Ham wanakaribia kufanikiwa kumnunua mshambuliaji wa Mexico Javier Hernandez kutoka kwa klabu ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani.
Klabu hiyo ina matumaini makubwa ya kufanikiwa kumchukua mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United, 29, ingawa kufikia sasa hawajakamilisha makubaliano kuhusu bei yake.
Hayo yakijiri, mshambuliaji wa Austria Marko Arnautovic anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu katika klabu hiyo katika saa 48 zijazo baada ya West Ham kuafikiana na Stoke City.
West Ham walikuwa wamewasilisha dau mara mbili zikikataliwa lakini sasa inaarifiwa Stoke wamekubali dau la karibu £24m.Hernandez alifunga mabao 59 katika mechi 156 alizochezea United tangu alipotua Old Trafford mwaka 2010, kabla ya kuhamia Leverkusen kwa£7.3m mwezi Agosti 2015.
Amefungia klabu hiyo ya Ujerumani mabao 39 katika mechi 76.
Arnautovic, 28, alijiunga na Stoke kutoka Werder Bremen miaka minne iliyopita na alikuwa ametumikia miezi 12 pekee mkataba wake wa sasa wa miaka minne klabu hiyo.
Alifunga mabao saba katika mechi 35 alizocheza mashindano yote msimu uliopita.
West Ham pia walifanikiwa kumsajili kipa wa England anayechezea Manchester City Joe Hart kwa mkopo wa mwaka mmoja Jumanne.
Mwezi Mei Hernandez - ambaye hujulikana sana kwa jina la utani la Chicarito, aliibuka kuwa mfungaji bora zaidi wa Mexico katika historia baada ya kufunga bao lake la 47.
Chapisha Maoni