Image result for SAMIA SULUHUMAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria dhidi ya waajiri wasiopeleka au kuchelewesha michango ya wanachama kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.
Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo jijini Mwanza juzi wakati anafungua semina ya maisha baada ya kustaafu, fursa ya mafao na uwekezaji, iliyoandaliwa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF).
Mafunzo hayo ni kwa ajili ya wastaafu watarajiwa 450 kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza. Makamu wa Rais alisema ni lazima kuchukua hatua hizo ili kukomesha tabia hiyo inayoathiri maslahi ya wanachama.
Alisisitiza kuwa waajiri wakichangia kwa mujibu wa sheria kwenye mifuko hiyo, watawezesha wanachama wao kupata mafao kikamilifu na kwa wakati. Kuhusu madeni ya Serikali kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini, Makamu wa Rais aliwahakikishia wakurugenzi wa mifuko hiyo kuwa Serikali inashughulikia madeni hayo na baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa madeni hayo, basi malipo yatafanyika haraka iwezekanavyo.
Makamu wa Rais alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha michango ya pensheni kwa wafanyakazi wa taasisi zinazopata ruzuku kutoka Serikalini inalipwa kwenye mifuko hiyo kwa wakati.
Aidha, Makamu wa Rais aliwahimiza wastaafu watarajiwa kote nchini, waache tabia ya kukata tamaa baada ya kustaafu, bali wajipange vyema na kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo viwanda vidogo, kilimo na biashara.
Makamu wa Rais alipongeza jitihada zinazofanywa na mfuko wa PSPF kwa kutoa mafunzo kwa wastaafu watarajiwa kwa ajili ya kuwasaidia kujipanga vyema pindi watakapostaafu utumishi wao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji aliwahakikishia wastaafu hao watarajiwa wa mkoa wa Mwanza kuwa Serikali itaendelea kusimamia vyema mifuko ya hifadhi ya jamii ili iweze kutoa mafao bora na kwa wakati.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top